Iran: Taarifa ya kikao cha Arab League haina maana wala itibari
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema taarifa ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) ni ya kipuuzi, isiyo na itibari na ambayo ni chachu ya fitina na migawanyiko katika eneo.
Bahram Qassemi mbali na kusisitiza kwamba sera za msingi na za kudumu za Jamhuri ya Kiislamu ni kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, amebainisha kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi ya Iran katika taarifa hiyo hazikubaliki.
Qassemi amebainisha kuwa ushawishi wa kimaanawi na kieneo wa Iran si suala ambalo linaweza kupunguzwa au kuzidishwa kwa njama za nchi moja au mbili na kwamba Iran itasogeza mbele siasa zake za kieneo na kimataifa kwa uhuru kamili ilionao.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, taarifa hiyo kama taarifa nyingine zilizopita imerudia tena madai hewa na uongo usio na tija dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na badala ya kutafuta sababu halisi za migogoro ya eneo la Mashariki ya Kati, kwa mara nyingine tena imeamua kuufumbia macho ukweli halisi wa mambo.
Katika taarifa iliyotolewa juzi mwishoni mwa kikao cha Kamati ya Pande 4 inayojumuisha Saudia, Imarati, Misri na Bahrain pambizoni mwa mkutano wa 151 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi wanachama wa Arab League, jumuiya hiyo ya nchi za Kiarabu ilirudia tena madai hewa dhidi ya Iran kwa kuitaka iache kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, huku ikiituhumu Tehran kuwa inapuuza sheria za kimataifa.
Kwa mujibu wa gazeti la Asharq al-Awsat la Saudia, taarifa hiyo imewatuhumu maafisa wa serikali ya Tehran kuwa wamekuwa wakitoa kauli za kichochezi dhidi ya nchi za Kiarabu, na kwamba Iran inaingilia masuala ya ndani ya Yemen.