Bunge la Iran lalaani mashambulizi ya kigaidi dhidi ya misikiti New Zealand
Wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran wametoa taarifa wakilaani mashambulizi ya kigaidi yaliyolenga misikiti nchini New Zealand na kuua shahidi makumi ya Waislamu waliokuwa wakitekeleza ibada ya Swala ya Ijumaa na kujeruhi makumi ya wengine.
Taarifa iliyotolewa leo Jumapili na Bunge la Iran imesema kuwa: Mashambulizi ya kigaidi ya New Zealand yamethibitisha kuwa, haki za binadamu na haki ya uhai wa mwanadamu vinatumiwa na mabeberu wa dunia kama wenzo wa kupeleka mbele malengo yao yasiyo ya kibinadamu.
Katika taarifa hiyo wabunge wa Iran wamesisitiza udharura wa kukabiliana na hatua yoyote inayotaka kutumia vibaya jina la Uislamu na Waislamu na kuzuia sera na misimamo ya kindumakuwili kuhusiana na magaidi.
Ijumaa iliyopita magaidi wenye chuki dhidi ya Uislamu walishambulia misikiti miwili ya Linwood na Al-Noor katika mji wa Christchurch nchini New Zealand na kuwamiminia risasi Waislamu waliokuwa wakiswali Swala ya Ijumaa. Katika hujuma hiyo ya kinyama Waislamu wasiopungua 49 waliuawa na wengine 50 kujeruhiwa. Nchi nyingi duniani na asasi za kimataifa hadi hivi sasa zinaendelea kulaani mashambulizi hayo.
Gaidi mwenye umri wa miaka 28 kwa jina Brenton Tarrant raia wa Australia ambaye alihusika katika shambulizi dhidi ya msikiti mmoja kati ya miwili iliyoshambuliwa nchini New Zealand amekuwa akijitangaza kuwa ni mfuasi wa sera za kibaguzi za Rais Donald Trump wa Marekani.