Idadi ya waliopoteza maisha katika mafuriko Iran yapindukia 40
Idadi ya watu waliopoteza maisha kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo kadhaa ya Iran imeongezeka na kufikia 42.
Hayo yalitangazwa jana Jumamosi na Mkuu wa Shirika la Dawa la Iran (FMOI), Ahmad Shojaei na kuongeza kuwa, miongoni mwa watu walioaga dunia katika mafuriko hayo ni wakazi 19 wa mji wa Shiraz, kusini mwa nchi.
Amesema watu wengine 7 wamepoteza maisha karibu na Ziwa Caspian katika mkoa wa Golestan, wawili katika mkoa wa Lorestan na wawili wawili katika mikoa ya Khuzestan, Kohgiluyeh na Boyer-Ahmad, Kermanshah, Hamedan na Semnan.
Habari zaidi zinasema kuwa, watu wengine watano wamekufa maji katika mkoa wa Mazandaran na wengine watatu katika mikoa ya Khorasan Razavi na Khorasan Kaskazini.

Hapo jana Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH), Muhammad Ali Jafari alizitembelea wilaya zilizoathiriwa zaidi na mafuriko hayo katika mkoa wa Golestan, ikiwa ni ziara ya pili ndani ya wiki moja katika maeneo hayo, kutathmini shughuli za kuwafikishia misaada ya kibinadamu waathiriwa wa janga hilo la kimaumbile.
Kufuatia mafuriko hayo, Gavana wa mkoa wa Khuzestan, Qolam-Reza Shariati amesema Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran Abdol-Reza Rahmani-Fazli, ameidhinisha kutangazwa hali ya hatari katika mkoa huo, huku kukiwa na wasiwasi wa kushuhudiwa mvua na mafuriko mengine.