Marekani ni hatari kubwa kwa mustakbali wa dunia
Mwanafikra wa Kiislamu kutoka visiwa vya Komoro amesema kuwa Marekai imehatarisha usalama wa dunia kutokana na siasa zake mbovu za kuingilia mara kwa mara mambo ya ndani ya nchi nyingine.
Tilaki Mahmoud msomi na mwanafikra wa Kiislamu wa Komoro aliyasema hayo jana Jumapili pambizoni mwa Kikao cha Kimataifa cha Mustakbali wa Ulimwengu wa Kiislamu ambacho kinafanyika hapa mjini Tehran. Kuhusiana na madai yasiyo na msingi ya watawala wa Marekani kwamba Iran inahatarisha usalama wa nchi za eneo la Asia Magharibi Tilaki Mahmoud amesisitiza kwamba Iran si tu kwamba sio tishio kwa usalama wa eneo na dunia bali tishio halisi ni Marekani ambayo ina tamaa kubwa ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine za dunia. Ameongeza kwamba miongoni mwa nchi zote za Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni mfano bora wa pekee katika nyanja zote za kiutamaduni, kielimu na kidini na kwamba nchi nyingine za Kiislamu zinapaswa kuichukulia Iran kuwa mfano wa kuigwa.
Mwanafikra huyo wa visiwa vya Komoro amesema kuwa nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kulinda na kueneza usalama katika ulimwengu wa Kiislamu haipingiki na kuongeza kuwa wafuasi wa dini nyinginezo wanaishi kwa amani na ndugu zao wa Kiislamu nchini Iran bila ya kuwa na wasiwasi wowote kuhusiana na usalama wao.
Kikao cha Kimataifa cha Mustakbali wa Ulimwengu wa Kiislamu katika upeo wa 1414 Shamsia, ambacho kinawashirikisha wanafikra wa Kiislamu kutoka nchi 10 za Kiislamu kilianza jana Jumapili katika Chuo Kikuu cha Tehran mjini Tehran na kinatazamiwa kukamilika leo Jumatatu.