Apr 29, 2019 10:16 UTC
  • Larijani: Wamarekani wafahamu kuwa Iran ni mshindani mgumu kwao

Spika wa Bunge la Iran, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Ali Larijani amesema Wairani kamwe hawatasalimu amri mbele ya wanaotumia mabavu na kuongeza kuwa: "Wakuu wa Marekani wanapaswa kufahamu kuwa, Iran ni mshindani mgumu kwao."

Ali Larijani, Spika wa Bunge la Iran ameyasema hayo Jumatatu  na kuashiria kuondoka Marekani katika mapatano ya nyuklia ya Iran yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji, JCPOA, na kusema: "Rais Donald Trump wa Marekani ni mtu wa ajabu ambaye kila siku anajiondoa katika mkataba wa kimataifa."

Larijani ameendelea kusema kuwa: "Hatua ambazo Trump anachukua zinaonyesha kuwa kuna hasara zinazopatikana katika uga wa kimataifa."

Spika wa Bunge la Iran aidha ameashiria masharti 12 ambayo Marekani imeweka kabla ya kufanya mazungumzo na Iran na kusema: "Sera za Marekani zimejengeka katika udhalilishaji na kuwalazimu wengine wasalimu amri na hii ndio hali ambayo Saudi Arabia iko nayo kwani imesalimu amri, ikatoa pesa na hatimaye ikadhalilishwa."

Larijani ameendelea kusema kuwa, taifa lenye ustaarabu na historia ndefu la Iran katu halitakubali masharti ya Marekani ya kufanya mazungumzo.

Ikumbukwe kuwa, mwezi Mei 2018, Rais Trump wa Marekani, alichukua hatua ya upande mmoja na kutangaza kujiondoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na akatangaza pia kurejesha vikwazo dhidi ya Iran.

Tags