Salehi: Iran hailazimiki tena kuchunga kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i53357
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema leo kwamba Tehran hailazimiki tena kuchunga kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa kwa asilimia 3.67 na vile vile kiwango cha tani 130 za maji mazito ya nyuklia.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
May 09, 2019 04:15 UTC
  • Salehi: Iran hailazimiki tena kuchunga kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa

Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema leo kwamba Tehran hailazimiki tena kuchunga kiwango cha kilo 300 za urani iliyorutubishwa kwa asilimia 3.67 na vile vile kiwango cha tani 130 za maji mazito ya nyuklia.

Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo mbele ya waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kuhusu uamuzi wa Iran wa kupunguza uwajibikaji wake katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA akisema: Kwa mujibu wa kifungu nambari 26 cha JCPOA, kila pale ambapo Iran itahisi kuwa upande wa pili haukutekeleza ahadi zake, Tehran nayo inaweza kupunguza uwajibikaji wake kwa baadhi ya ahadi za JCPOA ili kuufanya upande wa pili uangalie upya msimamo wake.

Amesema, Marekani imeikwamisha Iran kuuza urani yake iliyotubishwa wakati ambapo hiyo ni katika haki za Tehran kwa mujibu wa mapatano ya JCPOA. Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia hatua zilizochukuliwa na Marekani na kushindwa kuzibwa nafasi ya kujitoa Marekani katika mapatano hayo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anatangaza kwamba Iran haitouza trena urani yake iliyorutubishwa poamoja na maji mazito ya nyuklia hadi litakapotolewa tangazo jengine.

Miradi ya nyuklia ya Iran

 

Infaa kuashiria hapa kuwa, Iran imezifahamisha rasmi nchi tano zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kuhusiana na uamuzi wake wa kusimamisha kwa muda utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake kuhusu mapatano hayo, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Marekani kujitoa kwa upande mmoja katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa.

Leo Jumatano mabalozi wa nchi tano hizo yaani Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Russia na China mjini Tehran wamekabidhiwa barua iliyoandikwa na Rais Hassan Rouhani wa Iran kuhusiana na suala hilo. Barua hiyo imekabidhiwa mabalozi hao na Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran.