May 17, 2019 07:31 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran awasili China akitokea Japan

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili Beijing, mji mkuu wa China mapema leo Ijumaa katika safari yake ya kidiplomasia ya kuzitembelea nchi kadhaa za bara Asia.

Dakta Muhammad Javad Zarif anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa ngazi za juu wa China na kujadiliana nao kuhusu uhusiano wa pande mbili, masuala ya kieneo na kimataifa.

Safari ya Zarif mjini Beijing inajiri wakati huu ambapo vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaonekana kupamba moto.

China ni katika nchi muhimu zilizosalia kwenye makubaliano ya nyuklia ya Iran ya JCPOA, baada ya Washington kuchukua hatua ya upande mmoja na kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa Mei mwaka jana 2018.

Waziri Zarif (kushoto) na Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe

Mapema jana Alhamisi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alikutana na Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe na mwenzake wa nchi hiyo ya Asia, Taro Kono ambapo walijadili matukio ya hivi karibuni ya JCPOA na hatua za kisheria ambazo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imechukua kukabiliana na hatua ya Marekani ya kukiuka mapatano hayo na kuvunja sheria.

Kabla ya hapo, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alizitembelea India na Turkmenistan baada ya safari ya wiki iliyopita huko Moscow Russia.

Tags