Rais Rouhani: Iran bila shaka itapata ushindi katika makabiliano na Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mashinikizo ya kisiasa na kiuchumi ya Marekani dhidi ya Iran ya Kiislamu na kusema: "Taifa la Iran halijawahi na halitasalimu amri mbele ya mashinikizo."
Rais Rouhani aliyasema hayo Jumamosi usiku mjini Tehran wakati alipokutana na wakuu wa vyombo vya habari nchini. Katika kikao hicho, Rais Rouhani alisisitiza kuwa, Marekani haiwezi kuipigisha magoti Iran na kuongeza kuwa, bila shaka Iran itapata ushindi katika medani ya mapambano yake na Marekani.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia kujiondoa Marekani kinyume cha sheria katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kusema: "Leo nchi zote za dunia na taasisi za kimataifa zinaikosoa Marekani kwa kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.
Baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo ya nyuklia ambayo yanajulikana rasmi kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) ilizidisha mashinikizo ya pande zote dhidi ya Iran.
Mnamo Mei 8 2018, Rais Trump wa Marekani alichukua maamuzi ya upande mmoja na kukiuka ahadi za Marekani katika JCPOA na kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa sambamba na kurejesha vikwazo dhidi ya Iran. Hatua hii ya Marekani inaendelea kulaaniwa kimataifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu akizungumza 14 Mei katika mkutano na maafisa wa serikali, alisema chaguo lisilopingika la taifa la Iran ni kupambana na Marekani na katika makabiliano hayo, Marekani italazimika kulegeza msimamo na kurudi nyuma.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi sasa ina nafasi ya kimsingi katika eneo ya kukabiliana na njama za mhimili wa Marekani, Saudi na Utawala wa Kizayuni.