Iran iko tayari kufanya mazungumzo na nchi za Ghuba ya Uajemi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kufanya mazungumzo na kila moja ya nchi za Kiarabu za ukanda wa Ghuba ya Uajemi kuhusu masuala ya pande mbili na kieneo."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Sayyid Abbas Mousavi ameyasema hayo leo Jumatatu katika mkutano wa kila wiki na waandishi habari na katika kujibu swali la mwandishi wa Radio Tehran kuhusu madai ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Imarati (UAE) kuhusu udharura wa kushiriki nchi za Ghuba ya Uajemi katika mazungumzo ya Iran na nchi wanachama wa mapatano ya nyuklia yanayojulikana kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), amesema: "Pendekezo la Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kwa ajili ya kuundwa jukwaa la mazungumzo ya kieneo na kutiwa saini mapatano ya kutoshambuliana baina ya nchi za eneo ni mwanzo wa mazungumzo ya nchi za Ghuba ya Uajemi na Iran."
Hali kadhalika Sayyid Abbas Mousawi ameashiria matamshi dhidi ya Iran ya Rais Donald Trump wa Marekani na kusema: "Baada ya serikali ya Trump kujiondoa kinyume cha sheria katika JCPOA, haina ustahiki wa kuielekeza Iran inakotaka."
Ameongeza kuwa Marekani inawashinikiza watu wa Iran na kuwawekea vikwazo shadidi na wakati huo huo kudai kuwa inataka kufanya mazungumzo na Iran."

Mousavi pia amesema madai potovu ya rais wa Marekani ni sehemu ya vita vya kisaikolojia na kujaribu kuathiri fikra za umma. Ameongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeweza kusambaratisha mashinikizo ya kisaikolojia ya nchi za Magharibi kwa kushiriki katika mazungumzo ya JCPOA."
Kuhusu mchakato wa Iran kuwa na uhusiano wa kawaida na Ulaya, Mousavi amesema: "Tarajio la Iran kutoka kwa Umoja wa Ulaya lilikuwa ni nchi hizo kutekeleza ahadi zao katika JCPOA lakini hazikutaka au hazikuweza kufanya hivyo na hilo ni jambo la kusikitisha."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria safari tarajiwa ya Waziri Mkuu wa Japan Abe Shinzo mjini Tehran na kusema: "Safari ya kiongozi wa serikali ya Japan nchini Iran baada ya miaka 40 ni muhimu, ya kihistoria na ni ya kipekee."