Iran: Hatutarefusha muhula wa siku 60 wa EU kufungamana na JCPOA
(last modified Wed, 19 Jun 2019 12:45:53 GMT )
Jun 19, 2019 12:45 UTC
  • Iran: Hatutarefusha muhula wa siku 60 wa EU kufungamana na JCPOA

Msemaji wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema muda wa siku 60 ambao Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliupa Umoja wa Ulaya uwe umetekeleza ahadi zake za kufungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA hautarefushwa.

Behrouz Kamalvandi amesema hayo leo Jumatano na kuongeza kuwa, "Hatuwezi kuendelea kutekeleza wajibu wetu ilhali upande wa pili hautekelezi ahadi zake. Hatuwezi kurejea nyuma."

Amebainisha kuwa, "Ujumbe wetu uko wazi. Mienendo yao inaonesha kuwa ima hawataki kutekeleza majukumu yao au hawawezi kuyatekeleza. Sisi tutafuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na sheria za Majilisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge)." 

Kutokana na hali hiyo ya kulegalega nchi za Ulaya katika utekelezaji wa mfumo huo, Rais Hassan Rouhani wa Iran tarehe 8 mwezi uliopita alisema kwamba Tehran imesitisha utekelezaji wa baadhi ya vipengee vya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, kukiwemo kuongeza akiba ya urani yake iliyorutubishwa pamoja na maji mazito ya nyuklia.

Nchi zilizosalia kwenye JCPOA baada ya Marekani kujiondoa

Msemaji wa AEOI amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuanzia Juni 27 itapitisha kiwango cha urutubishaji wa urani mara nne zaidi, na kwamba akiba yake ya urani itapita kiwango cha kilo 300 kilichoanishwa kwenye makubaliano ya nyuklia kufikia tarehe hiyo.

Tayari  Iran imezifahamisha rasmi nchi tano (4+1) zilizosalia katika mapatano ya nyuklia ya mwaka 2015 mashuhuri kama Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji JCPOA kuhusiana na uamuzi wake wa kusimamisha kwa muda utekelezaji wa baadhi ya ahadi zake kuhusu mapatano hayo, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya Marekani kuchukua hatua ya upande mmoja ya kujiondoa katika mapatano hayo muhimu ya kimataifa.

Tags