Iran yamuita balozi wa Nigeria nchini kuhusu hali ya Sheikh Zakzaky
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imemuita balozi mdogo wa Nigeria hapa mjini Tehran na kumkabidhi malalamiko rasmi pamoja na kumueleza wasiwasi wa taifa hili kuhusu ripoti zinazoashiria kuwa mbaya zaidi hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria.
Msemaji wa wizara hiyo, Abbas Mousavi amesema kikao hicho kilifanyika jana Jumatatu na kwamba Iran imemfahamisha bayana mwanadiplomasia huyo wa Nigeria kuhusu kuendelea kudorora afya ya mwanazuoni huyo mashuhuru wa Waislamu wa Kishia.
Amesema, "Tunatumai kuwa, jitihada zinachokuliwa kwa ajili ya kuimarisha hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky zitazaa matunda na kiongozi huyo wa Kiislamu atarejea katika hali yake nzuri ya afya."
Haya yanajiri siku chache baada ya Taasisi ya Kimataifa ya Haki za Binadamu ya Solh-e Ziba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kumuandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kuutaka umoja huo uandae haraka mazingira ya kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky.
Barua hiyo imesema kuwa, kwa mujibu wa taarifa za kina na za uhakika za wataalamu wa asasi za kijamii na mashirika ya kimataifa ya haki za binadamu, hali ya kiafya ya Sheikh Ibrahim Zakzaky ni mbaya hasa baada ya kuibuka madai kuwa amedungwa sumu mwilini, na kwamba kutishia usalama wa maisha ya kiongozi huyo kunaweza kusababisha hatari za kiusalama na uvunjifu wa amani katika sehemu mbalimbali duniani.
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria anashikiliwa na jeshi na serikali ya Nigeria tangu mwaka 2015 baada ya kupigwa risasi wakati wanajeshi wa nchi hiyo walipovamia nyumba yake mjini Zaria na kuua mamia ya Waislamu.