Maulamaa wa Iran waitaka Nigeria imuachie huru Sheikh Zakzaky
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54791-maulamaa_wa_iran_waitaka_nigeria_imuachie_huru_sheikh_zakzaky
Jumuiya ya Wanazuoni wa Hauza ya Kidini ya Qom hapa nchini Iran sambamba na kulaani kuendelea kushikiliwa korokoroni katika mazingira mabaya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi Nigeria, wameitaka serikali ya Abuja imuachie huru kiongozi huyo wa Waislamu ya madhehebu ya Shia.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 16, 2019 02:44 UTC
  • Maulamaa wa Iran waitaka Nigeria imuachie huru Sheikh Zakzaky

Jumuiya ya Wanazuoni wa Hauza ya Kidini ya Qom hapa nchini Iran sambamba na kulaani kuendelea kushikiliwa korokoroni katika mazingira mabaya Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchi Nigeria, wameitaka serikali ya Abuja imuachie huru kiongozi huyo wa Waislamu ya madhehebu ya Shia.

Jumuiya hiyo imetoa mwito huo katika taarifa yao ya jana Jumatatu na kuongeza kuwa, "Serikali ya Nigeria haikutosheka na kumzuilia kinyume cha sheria Sheikh Zakzaky, bali imeenda mbali zaidi na kula njama ya kumpa sumu, ili ichochee hasira na ghadhabu za Waislamu wa nchi hiyo ya Afrika Magharibi."

Wanazuoni wa Hauza ya Qom hapa nchini wameeleza bayana kuwa, ni jambo la kusikitisha kuwaona wale wanaojinadi kuwa watetezi wa haki za binadamu duniani wameunyamazia kimya ukatili na mateso anayokumbana nayo msomi huyo wa Kiislamu wa Nigeria mikononi mwa vyombo vya usalama.

Taarifa ya Jumuiya ya Wanazuoni wa Hauza ya Kidini ya Qom hapa nchini Iran imeeleza kuwa, "Hatua zisizo za kiutu na zilizo kinyume na sheria za serikali ya Nigeria zinaungwa mkono na Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa Aal-Saud wa Saudi Arabia, na ndiposa wahusika wa vitendo hivyo hawajachukuliwa hatua zozote za kisheria. Jeshi la Nigeria limewaua shahidi Waislamu wengi wa Nigeria wakiwemo watoto wadogo."

Wanachuo wa Iran wakitaka kuachiwa huru Sheikh Zakzaky

Wanazuoni wa Kiislamu nchini wametoa taarifa hiyo masaa machache baada ya wanachuo wa vyuo vikuu hapa mjini Tehran kufanya mkusanyiko mkubwa kulalamikia kuendelea kushikiliwa Sheikh Zakzaky, ambapo pia wamelaani vikali kimya cha jamii ya kimataifa hususan Umoja wa Mataifa kuhusiana na ukiukaji wa haki za binadamu dhidi ya Waislamu wa Kishia nchini Nigeria.

Licha ya Mahakama Kuu ya Nigeria kutoa amri ya kuachiliwa huru mara moja mwanachuoni huyo mwezi Disemba 2016 na kuliwajibisha jeshi la nchi hiyo kuilipa familia ya Sheikh Zakzaky fidia ya dola laki moja na 50 elfu, lakini vyombo vya dola vya Nigeria vimekataa kabisa kutekeleza amri hiyo ya mahakama na hadi hivi sasa mwanaharakati huyo wa Kiislamu anaendelea kushikiliwa korokoroni kinyume cha sheria tokea Disemba 2015.