Azma ya taifa la Iran; kutosalimu amri mbele ya maadui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i54999-azma_ya_taifa_la_iran_kutosalimu_amri_mbele_ya_maadui
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sepah, amesema kuwa hakuna nguvu yoyote inayoweza kuichukulia uamuzi Iran na kwamba ulimwengu unapasa kuheshimu rasmi irada na azma ya taifa la Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 26, 2019 05:38 UTC
  • Azma ya taifa la Iran; kutosalimu amri mbele ya maadui

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Sepah, amesema kuwa hakuna nguvu yoyote inayoweza kuichukulia uamuzi Iran na kwamba ulimwengu unapasa kuheshimu rasmi irada na azma ya taifa la Iran.

Akizungumza siku ya Alkhamisi mbele ya umati mkubwa wa wanajihadi wa mkoa wa Khuzestan kusini magharibi mwa Iran, Kamanda Mkuu Hussein Salami amesema kuwa hakuna mtu yoyote anayeweza kuilazimisha Iran kufuata matakwa yake na kuongeza kuwa, maadui hawapasi kufanya makosa katika mahesabu yao kuhusiana na Iran, na ni lazima watambue kuwa taifa la Iran ni mwalimu mkubwa na mahiri wa mapambano, na kutumia mashinikizo, mzingiro na vitisho sio njia ya kukabiliana na taifa hili.

Kutokana na kutetea maslahi yake kwa uhuru kamili, Iran daima imekuwa ikikabiliwa na propaganda chafu, vita vya kisaikolojia na hata vitisho vya maadui.

Azma na ukakamavu wa Iran mbele ya madola makubwa na yenye kiburi duniani yakiongozwa na Marekani, umelifanya taifa hili kupita salama na kwa mafanikio katika vizingiti na mitego hatari ya maadui katika uhai wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ni wazi kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yameudhihirishia wazi ulimwengu, funzo la 'mapambano', 'kusimama imara', 'ukakamavu' na 'kujitolea' kwa taifa la Iran.

Mapinduzi ya Kiislamu yamethibitisha kwamba kujitawala kumeliunganisha taifa la Iran na ndio maana maadui wameshindwa kulidhuru taifa hili katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.

Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Sepah

Kuhusiana na suala hili. Carlos Santa Maria, mtaalamu wa masuala ya siasa wa Colombia amesema katika mahijiano na Idhaa ya Kihispania ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba, nchi ambazo zinajitawala kikamilifu kamwe hazitasalimu amri mbele ya adui.

Kutosalimu amri ni sifa thabiti ya taifa la Iran tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na leo pia sifa hiyo imebadilika na kuwa mfano unaoigwa na mataifa mbalimbali yanayopigania uhuru na kujitawala kwao duniani. Sababu ya uadui huu wote ambao umekuwa ukifanywa na watawala tofauti wa Marekani dhidi ya taifa la Iran ni kusimama imara taifa hili mbele ya njama tofauti za maadu na hatimaye kuzivunja zote.

Miaka minane ya vita vya kulazimishwa vya utawala wa kidikteta wa Saddam wa Iraq dhidi ya Iran na mapambano makali yaliyoonyeshwa na wapiganaji wa taifa la Iran katika vita hivyo yalithibitisha wazi ukakamavu usioshindwa wa taifa la Iran na kuonyesha kuwa taifa hili kamwe haliwezi kushindwa kwa kutumiwa mashinikizo, vikwazo na vitisho vya maadui.

Ni irada na azma hiyo thabiti na madhubuti ya taifa la Iran ndiyo imemchanganya Rais Donald Trump wa Marekani na kumfanya asijue la kufanya katika kukabiliana na taifa hili shupavu.

Trump ambaye ameanika wazi uadui wake mkubwa dhidi ya taifa la Iran tokea aingie madadarakani nchini Marekani amekuwa akitumia mbinu tofauti za vikwazo, mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi na vitisho ili kulifanya taifa la Iran limpigie magoti lakini ameshindwa kufikia lengo lake hilo kutokana na 'mapambano ya kiwango cha juu zaidi' ya taifa la Iran.

Mbali na hayo, jibu kali lililotolewa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran Sepah, kwa ndege isiyo na rubani ya Marekani Global Hawk iliyokuwa imekiuka unga ya Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi, limeikejeli nguvu ya kijeshi na kiteknolojia ya Marekani.

Global Hawk, droni ya kisasa kabisa ya Marekani iliyotunguliwa na jeshi la Sepah

Kuhusiana na kuangushwa kwa ndege hiyo, Carlos Santa Maria anasema: Madai ya Marekani kufikia ubora wa juu zaidi wa teknolojia hayana maana tena na nchi zinazostawi zimefikia kiwango cha juu cha teknolojia ya mawasiliano kiasi kwamba si tu kuwa zinajua namna ya kujilinda bali zina uwezo wa kufikia kiwango cha juu zaidi cha teknolojia.

Licha ya kuwepo vikwazo na mashinikizo ya aina tofauti ya maadui, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imebadilika kuwa nguvu kubwa ya kieneo, nguvu ambayo inazidi kuimarika siku baada ya nyingine.

Msimamo unaobadilika wa serikali ya Donald Trump kutoka kwenye vitisho na kuamua kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bila shaka unatokana na kukataa tamaa serikali hiyo na kutosalimu amri taifa lenye umoja la Iran.