Zarif: Marekani inahofia kushindwa katika uga wa diplomasia
(last modified Sun, 11 Aug 2019 04:01:32 GMT )
Aug 11, 2019 04:01 UTC
  • Zarif: Marekani inahofia kushindwa katika uga wa diplomasia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa Marekani ina wasiwasi na kuhofia kushindwa katika uga wa diplomasia.

Muhammad Javad Zarif jana Jumamosi alikutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) hapa Tehran. Dakta Zarif alisisitiza jinsi Marekani inavyoishinikiza Iran kutokana na nguvu na uwezo wa nchi hii na kueleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanikiwa katika uga wa kieneo na kimataifa. 

Kwa upande wao, wabunge  wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran walishukuru na kupongeza jitihada za kiongozi huyo anayehusika na siasa za nje za Iran na kulaani hatua ya Marekani ya kumuwekea vikwazo Muhammad Javad Zarif.  Wizara ya Fedha ya Marekani ambayo imegeuka na kuwa chumba cha kuendeshea vita vya kiuchumi vya White House dhidi ya wananchi wa Iran tarehe Mosi mwezi huu wa Agosti ililiweka jina la Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika orodha yake ya vikwazo. 

Kabla ya mazungumzo ya Zarif na wabunge hao, baadhi ya wakurugenzi wa magazeti kote nchini Iran waliitembelea Wizara ya Mambo ya Nje mjini Tehran na kupongeza juhudi zinazofanywa na Muhammad Javad Zarif katika kutetea maslahi ya taifa la Iran katika ngazi za kimataifa. Wakurugenzi hao wa magazeti nchini Iran aidha walilaani  hatua ya Marekani ya kumuwekea vikwazo Zarif  na kutangaza kumuunga mkono Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Iran. 

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran pia hivi karibuni aliitembelea Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif. 

Dakta Zarif (kulia) katika mazungumzo na Ali Larijani