Rais Rouhani: Iran haina ajenda ya kufanya mazungumzo na Marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Iran haijawahi kuwa na ajenda ya kufanya mazungumzo ya pande mbili na Marekani.
Akihutubia Bunge mapema leo, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, kusimama kidete ndani ya nchi na diplomasia amilifu ndiyo stratijia ya serikali ya Iran na kuongeza kuwa: Maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu wanajua vyema kwamba, vita vya kutishwa vya uchumi vya Marekani dhidi ya Iran vitashindwa kama ilivyokuwa katika vita vya kutwisha vya kijeshi vya kabla ya miaka 30 iliyopita.
Rouhani amesema kuwa, stratijia ya Iran mkabala wa Marekani ni kuwa na subira ya kimapinduzi na tadbiri ya kimantiki na kuongeza kuwa: Kwa kutumia stratijia hiyo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubakia peke yake katika medani ya kimataifa na kinyume chake, imeifanya Marekani itengwe.
Rais Rouhani amesema, baada ya mwaka mmoja wa subira ya kistratijia siasa za kupunguza utekelezaji wa majukumu ya Iran katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zimeanza na kwamba iwapo Ulaya haitatekeleza majukumu yake katika makubaliano hayo, Jamhuri ya Kiislamu itachukua hatua ya tatu ya kupunguza utekelezaji wa majukumu yake.
Tarehe 8 Mei 2019, Iran ilianza kupunguza kiwango cha utekelezaji wa majukumu yake ndani ya mapatano ya nyuklia ya JCPOA kwa mujibu wa vifungu vya 26 na 36 vya makubaliano hayo. Tarehe 7 Juni mwaka huu pia, Iran ilianza kurutibisha urani kwa zaidi ya asilimia 3.67.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetangaza kuwa, kuanzia tarehe 6 Septemba 2019 itaanza kutekeleza awamu ya tatu ya kupunguza utekelezaji wa majukumu yake ndani ya JCPOA iwapo nchi za Ulaya zitashindwa kutekeleza majukumu yao.