Qalibaf: Utawala wa Kizayuni kwa mara nyingine tena umeonesha dhati yake ya kijinai
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, jinai za utawala wa Kizayuni katika miji ya Beirut na Tehran na kuendelea kuwaua watoto huko Ghaza, kwa mara nyingine tena zimewaonesha walimwengu dhati halisi ya kijinai, ukatili na ubeberu wa dola hilo pandikizi.
Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA; Katika ujumbe kwa Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, Mohammad Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran sambamba na kutoa rambirambi za kuuawa shahidi Jenerali Fouad Shukr, mmoja wa makamanda wa Hizbullah ameandika: Utawala wa Kizayuni unajaribu kufidia kushindwa kwake na kuficha jinai zake huko Ghaza kupitia kuwaua kigaidi makamanda wa muqawama ili kuzuia uungaji mkono kwa wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.
Spika Qalibaf aidha amesema: Jinai za utawala wa Kizayuni katika miji ya Beirut na Tehran ya siku chache zilizopita na kuendelea kuwaua watoto huko Ghaza zimezidisha mafaili meusi katika historia iliyojaa ukatili na jinai ya utawala wa Kizayuni.
Jioni ya Jumanne ya tarehe 23 Julai, utawala wa Kizayuni ulishambulia jengo moja la ghorofa la makazi ya raia wa kawaida katika viunga vya mji wa Beirut huko Lebanon kwa makombora matatu na kumuua shahidi Fuad Shukr, mmoja wa makamanda wa ngazi za juu wa harakati ya Hizbullah ya Lebanon. Mshauri mmoja wa kijeshi wa Iran pia aliuawa shahidi kwenye jinai hiyo.