Meja Jenerali Salami: Mashinikizo ya maadui hayawezi kuipigisha magoti Iran
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) amesema kuwa, taifa la Iran limedhihirisha kuwa lina nguvu kuliko vikwazo na katu haliwezi kupigishwa magoti na mashinikizo ya maadui.
Meja Jenerali Hussein Salami aliyasema hayo jana katika mji wa Aq Qala mkoani Golestan kaskazini mwa nchi na kueleza bayana kuwa, "Mashinikizo ya maadui yamewafanya Wairani wapate nguvu zaidi."
Amesema vikwazo na mashinikizo hayajakuwa na matokeo mengine ghairi ya kuwashajiisha na kuwapa uimara Wairani, sambamba na kuwapa ari ya kuendelea kulijenga taifa lao.
Meja Jenerali Hussein Salami amebainisha kuwa, "Sisi ni taifa moja lililoungana, lenye azma thabiti na uongozi imara."
Kamanda Mkuu wa IRGC amesisitiza kuwa, Iran katu haitasalimu amri katika mazingira yoyote yale na kuongeza kwamba, mashinikizo na vikwazo si njia ya kukabiliana na Iran.
Marekani imeshadidisha mashinikizo na vikwazo vyake vya kidhalimu dhidi ya wananchi wa Iran tokea mwaka jana, baada ya Rais Donald Trump kuiondoa nchi hiyo kwenye makubalinao ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA.