Iran: Uchu wa madaraka wa 'Hitler mdogo' chachu ya kuangamizwa mapema Israel
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amemtaja Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, kama 'Hitler mdogo' na kusisitiza kuwa uchu wa madaraka wa Benjamin Netanyahu utakuwa mwanzo wa kuporomoka na kusambaratika utawala huo haramu.
Hossein Amir-Abdollahian alisema hayo jana Jumamosi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, matamshi ya vitisho na yasiyo na mantiki ya Netanyahu ni sehemu ya njama za Marekani na Israel dhidi ya Wapalestina kwa jina la 'Muamala wa Karne'.
Abdollahian ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amebainisha kuwa, "Hitler mdogo anafanya jitihada za kuanzisha vita katika eneo kwa uungaji mkono wa utawala wa (Donald) Trump na kwa kutumia pesa za nchi fulani zenye utajiri wa mafuta."
Hata hivyo amesisitiza kuwa iwapo tawala hizo zitathubutu kufuata mkondo huo wa vita, bila shaka zitatiwa adabu na wanamapambano wa Palestina kwa kucheza na moto.
Kadhalika Amir-Abdollahian ametoa mwito kwa nchi za Kiislamu na jamii ya kimataifa kukabiliana na harakati haribifu za utawala wa Kizayuni wa Israel zinazoyumbisha usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi.
Aidha Katibu Mkuu wa Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Intifadha ya Palestina amelaani vikali njama mpya za Wazayuni za kutaka kupora sehemu ya ardhi ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuiunganisha na ardhi zilizoghusubiwa za Palestina; na kueleza bayana kuwa mpango huo batili wa Netanyahu unaolenga kumbakisha madarakani utakuwa chachu ya kusambaratishwa mapema utawala huo haramu.