Rouhani: Nchi za Ulaya zimekiri hazijui aliyeshambulia Aramco
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56284-rouhani_nchi_za_ulaya_zimekiri_hazijui_aliyeshambulia_aramco
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema licha ya nchi za Ulaya kuituhumu Tehran kuwa imehusika katika mashambulizi yaliyolenga kituo kikubwa cha kusafisha mafuta cha Aramco nchini Saudi Arabia, lakini viongozi wa nchi hizo wamekiri wazi kuwa hawajui ni nani aliyetekeleza hujuma hizo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 27, 2019 23:10 UTC
  • Rouhani: Nchi za Ulaya zimekiri hazijui aliyeshambulia Aramco

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema licha ya nchi za Ulaya kuituhumu Tehran kuwa imehusika katika mashambulizi yaliyolenga kituo kikubwa cha kusafisha mafuta cha Aramco nchini Saudi Arabia, lakini viongozi wa nchi hizo wamekiri wazi kuwa hawajui ni nani aliyetekeleza hujuma hizo.

Rais Rouhani alisema hayo jana Ijumaa baada ya kuwasili hapa nchini akitokea New York, alikoenda kushiriki mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kufafanua kuwa, "Katika mazungumzo yangu na viongozi wa nchi kadhaa za Ulaya, niliwabana wanipe ushahidi wa madai yao dhidi ya Iran, lakini walishindwa na kukiri kuwa hawajui ni nani haswa alitekeleza mashambulizi hayo."

Dakta Rouhani ameongeza kwa kusema: "Niliwaeleza bayana kuwa, mna taarifa nyingi kuhusu maadui wa Yemen kwa kuwa mnawauzia silaha, lakini hamna ufahamu wowote kuhusu uwezo wa Wayemen au Mahouthi (Harakati ya Ansarullah)."

Rais Rouhani amezionya nchi hizo za Ulaya dhidi ya kutoa madai ya aina hiyo yasiokuwa na msingi wowote na kuwafahamisha kuwa, matamshi yanayotolewa bila ushahidi au ithibati ndicho kitu kinachofahamika kama madai au tuhuma.

Mashambulio ya Septemba 14 dhidi ya vituo vya mafuta vya Saudia

Septemba 23, viongozi wa nchi hizo tatu za Ulaya, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Chansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Uingereza, Borris Johnson walitoa taarifa ya pamoja pambizoni mwa mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, iliyoibebesha Iran dhima ya mashambulizi hayo ya Septemba 14, na kusisitiza kuwa eti wanaunga mkono uchunguzi unaoendelea juu ya hujuma hizo.

Hii ni katika hali ambayo, kikosi cha drone cha jeshi na wapiganaji wa kujitolea wa Yemen kimetangaza kuwa ndicho kilichohusika na shambulio dhidi ya vituo vya mafuta vya shirika la mafuta la Aramco katika viwanda vya kusafisha mafuta vya Abqaiq na Khurais vilivyoko mashariki ya Saudi Arabia.