Kiongozi Muadhamu: Mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani yamefeli
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56379-kiongozi_muadhamu_mashinikizo_ya_kiwango_cha_juu_ya_marekani_yamefeli
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kufeli siasa za Marekani za kuiwekea Iran mashinikizo makubwa kupindukia na kutosalimu amri Tehran mbele ya mashinikizo ya mfumo wa kibeberu akisisitiza kuwa, Iran itaendelea kwa nguvu zote kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA hadi itakapofikia lengo lililokusudiwa.
(last modified 2026-08-17T09:53:57+00:00 )
Oct 02, 2019 08:48 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Mashinikizo ya kiwango cha juu ya Marekani yamefeli

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia kufeli siasa za Marekani za kuiwekea Iran mashinikizo makubwa kupindukia na kutosalimu amri Tehran mbele ya mashinikizo ya mfumo wa kibeberu akisisitiza kuwa, Iran itaendelea kwa nguvu zote kupunguza ahadi zake ndani ya JCPOA hadi itakapofikia lengo lililokusudiwa.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo (Jumatano) wakati alipoonana na maelfu ya makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Amegusia pia njama zilizofeli hivi karibuni za Marekani za kujaribu kuonesha kuwa Iran imeshindwa na imesalimu amri mbele ya mashanikizo hayo na kuongeza kuwa, Wamarekani wamefikia hata kumbembeleza kwa kila namna Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili akubali kuonana nao na wawaoneshe walimwengu kuwa Iran imeshindwa na imesalimu amri. Wamefikia hata kutumia marafiki wao wa Ulaya lakini hadi hivi sasa wameshindwa na napenda kukuhakikishieni kuwa kamwe hawatofanikiwa.

Ameashiria pia kadhia ya nyuklia na kusema, suala la kupunguza ahadi za nyuklia limo mikononi mwa Taasisi ya Nishati ya Nyuklia ya Iran. Taasisi hiyo inapaswa kuendelea kutekeleza vilivyo, kwa kina na kikamilifu yale yote yanayotangazwa na serikali hadi yatakapopatikana matunda yaliyokusudiwa na bila ya shaka yoyote matunda hayo yatapatikana.

Mkutano wa leo Jumatano, Oktoba 2, 2019 wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na makamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH)

 

Ayatullah Khamenei amezungumzia pia hasara kubwa wanayopata maadui hasa Marekani huko Afghanistan, Iraq na Syria na kusisitiza kuwa, mabeberu wametumia fedha nyingi kuunda genge la Daesh (ISIS) na kuliunga mkono kikamilifu kisilaha, kifedha na kipropaganda, lakini hivi sasa kutokana na hima ya vijana wa Syria, Iraq na Iran, genge la Daesh limeangamizwa, lakini utawasikia mabeberu hao wanaeneza uongo wakidai kuwa eti wao ndio walioliangamiza genge hilo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amepongeza uwezo wa majimui adhimu ya muqawama katika kupambana na kambi ya kufru na dhulma na kutoa nasaha kwa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (SEPAH) akisema: Hakikisheni mnaulinda mtazamo wenu mpana unaoangalia hadi nje ya mipaka ya Iran kuhusu jiografia ya kambi ya muqawama.