Iran kuzindua satalaiti tatu mpya za Zafar, Pars 1 na Nahid 1
Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran itakamilisha utengenezaji wa satalaiti tatu mpya katika kipindi cha miezi mitatu ijayo.
Dakta Murtadha Barari ameyasema hayo leo Jumamosi mjini Tehran wakati akizungumza na waandishi habari kwa munasaba wa kuanza Wiki ya Kimataifa ya Anga za Mbali. Amesema utengenezaji wa satalaiti tatu mpya utakamilika katika kipindi cha miezi mitatu ijayo na baadaye kurushwa katika anga za mbali. Amezitaja satalaiti hizo kuwa ni Zafar, Pars 1 na Nahid 1.
Akiashiria kufeli baadhi ya sataliti ambazo Iran imezirusha katika anga za mbali, Mkuu wa Shirika la Anga za Mbali la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, katika miaka 3 ya kwanza ya Marekani kuanza harakati zake katika anga za mbali, sataliti zake 27 kati ya 43 ilizorusha katika anga za mbali zilifeli.
Ameongeza kuwa, sataliti 5 kati ya 11 ambazo Russia pia mwanzoni ilituma katika anga za mbali zilifeli. Dkt. Barari amesema kuwa, kwa mujibu wa takwimu asilimia 40 ya satalaiti za Iran zimefanikiwa kufika katika anga za mbali.
Iran ilirusha katika anga za mbali satalaiti yake ya kwanza kabisa inayojulikana kama Omid (yaani Tumaini) mwaka 2009. Iran pia imetangaza kuwa katika kipindi cha miaka michache ijayo itatuma mwanadamu katika anga za mbali.