Mousavi: Iraq na Syria ziliisambaratisha kitambo ISIS kwa msaada wa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i56909-mousavi_iraq_na_syria_ziliisambaratisha_kitambo_isis_kwa_msaada_wa_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) lilisambaratishwa na Iraq na Syria muda mrefu umepita, kwa msaada wa kilojistiki wa Jamhuri ya Kiislamu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Oct 28, 2019 12:21 UTC
  • Mousavi: Iraq na Syria ziliisambaratisha kitambo ISIS kwa msaada wa Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) lilisambaratishwa na Iraq na Syria muda mrefu umepita, kwa msaada wa kilojistiki wa Jamhuri ya Kiislamu.

Sayyid Abbas Mousavi amegusia habari ya kuuawa kiranja wa kundi hilo la ukufurishaji, Abubakr al-Baghdadi katika operesheni ya jeshi la Marekani na kusisitiza kuwa, "Magaidi kama Abubakr al-Baghdadi waliundwa, kupewa mafunzo na kuungwa mkono kwa hali na mali na Marekani, na mara tu muda wao wa kutumiwa unapomalizika, wao hufutwa mara moja katika taswira."

Ameeleza bayana kuwa, kundi la ISIS lilisambaratishwa zamani na vijana wanamuqawama wa Iraq na Syria kwa uungaji mkono wa kilojistiki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mousavi ameonya kuwa, ingawaje kundi la Daesh limeangamizwa kwa ushirikiano wa nchi za eneo, lakini moyo wake ungali hai na yumkini Marekani ikatumia mabaki ya magaidi hao kulihuisha genge hilo na kupanga njama mpya dhidi ya eneo.

Abubakar al-Baghdadi, kikaragosi wa Marekani aliyeuawa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, kuuawa Baghdadi si jambo kubwa kama linavyokuzwa na vyombo vya habari vya Wamagharibi, na kwamba Marekani imekuwa ikitumia karata ya aina hii kila unapokaribia uchaguzi nchini humo.

Amesema nchi za Asia Magharibi zinapaswa kuwa macho kutokana na fitina na njama mpya zitakazopikwa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya eneo hili.