Iran: Baraza la Usalama la UN linakabiliwa na migogoro ya uhalali na itibari, linahitaji mageuzi
(last modified Tue, 26 Nov 2019 08:06:59 GMT )
Nov 26, 2019 08:06 UTC
  • Iran: Baraza la Usalama la UN linakabiliwa na migogoro ya uhalali na itibari, linahitaji mageuzi

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema, Baraza la Usalama la umoja huo linakabiliwa na migogoro ya uhalali na itibari ambayo inapasa ishughulikiwe kwa kufanyiwa mageuzi baraza hilo.

Majid Takht-Ravanchi ameyasema hayo katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika kwa anuani ya "Suala la uwakilishi wa usawa na kuongezwa idadi ya wanachama wa Baraza la Usalama pamoja na masuala husika."

Takht-Ravanchi amekosoa muundo wa Baraza la Usalama lenye wanachama 15, likiwa linahodhiwa zaidi na nchi za Magharibi na kusisitizia haja ya kupanuliwa kwa namna itakayoleta mlingano.

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, kijiografia, Baraza la Usalama limehodhiwa zaidi na nchi za Magharibi, ambapo tatu miongoni mwao zina kura ya veto; na kwa upande wa kijiografia, wakati nchi hizo za Magharibi na kundi jengine moja zina uwakilishi mkubwa, maeneo mengine ya dunia yana uwakilishi duni kwa mtazamo wa kiidadi, na vilevile yana haki na manufaa chache kwa upande wa nguvu ya kura ya turufu au uanachama wa kudumu.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Ameongeza kuwa: Hadi kufikia leo theluthi moja ya wanachama wa Umoja wa Mataifa hawajawahi kupata fursa ya kuwa wanachama wa Baraza la Usalama, wakati kuna nchi 20 ambazo kila moja imeshawahi kuwa mwanachama katika baraza hilo kwa miaka 10 hadi 22.

Takht-Ravanchi amesisitiza kuwa utovu huo wa mlingano na haki inapasa ushughulikiwe na kufanyiwa marekebisho ikiwemo kuwekewa kikomo cha fursa kwa nchi zilizohudumu mara nyingi zaidi, na badala yake kutoa fursa na upendeleo kwa nchi ambazo hazijawahi kabisa au zilizohudumu mara chache katika Baraza la Usalama.

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema "uadilifu" na "sheria za kimataifa" ndio misingi miwili mikuu ya kupimia utendaji na ufanisi wa Baraza la Usalama na akasisitiza kwamba: "Kwa kutumia vigezo hivi viwili katika kutathimini utendaji wa baraza kuhusiana na eneo letu inadhihirika wazi kuwa, katika takribani kadhia zote, kuanzia mgogoro wa muda mrefu zaidi katika eneo letu, yaani kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu kinyume cha sheria Palestina na baadhi ya maeneo ya Syria na Lebanon, uvamizi wa Saddam dhidi ya Iran, uvamizi wa Marekani dhidi ya Iraq hadi kwenye mzingiro usio wa kibinadamu dhidi ya Ukanda wa Gaza pamoja na kuanzishwa mgogoro na hali mbaya zaidi ya kibinadamu duniani nchini Yemen, misingi ya "uadilifu" na "sheria" imekosekana kikamilifu".../