Kuanza uandikishaji wa wagombea uchaguzi wa Bunge la 11 la Iran
Uandikishaji watu wanaotaka kugombea ubunge katika uchaguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, yaani Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ulianza rasmi jana Jumapili na utaendelea hadi tarehe 7 ya mwezi huu wa Desemba.
Wale wote wanaotaka kugombea, wakiwa na hati na vitambulisho vinavyohitajika kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, wanatakiwa wajaze fomu maalumu ya uandikishaji ili kuthibitisha azma yao ya kutaka kuwania nafasi ya ubunge.
Februari mwaka 2020 ndipo utapofanyika uchaguzi wa Bunge la 11 katika majimbo 208 ya uchaguzi kote nchini kwa ajili ya kuwachagua wabunge 290 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na utafanyika pia uchaguzi mdogo wa Baraza la Tano la Wanazuoni Wataalamu wa Kumchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi katika majimbo matano ya Tehran, Fars, Khorasan ya Kaskazini, Khorasan ya Razavi na Qum.
Kufanyika uchaguzi ni moja ya misingi ya ushirikishaji umma kisiasa na kuwa na utawala unaotokana na ridhaa ya wananchi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 62 ya Katiba, Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu inaundwa kutokana na wawakilishi wa wananchi, ambao huchaguliwa moja kwa moja kwa kura za siri kwa kipindi cha miaka minne.
Uchaguzi nchini Iran unafanyika kwa kufuata taratibu na misingi miwili mikuu ya uendeshaji na usimamizi. Kwa upande wa uendeshaji na kulingana na katiba, Wizara ya Mambo ya Ndani ndiyo inayoratibu na kupanga sheria na kanuni za uendeshaji uchaguzi, namna ya utekelezaji wa awamu za uchaguzi, kusimamia upigaji kura na kuzihesabu pamoja na kuthibitisha kuwa uchaguzi unafanyika kama inavyotakikana katika kila kituo.
Kwa muktadha huo, kuna masharti jumla na masharti maalumu yaliyowekwa katika sheria ya uchaguzi wa wabunge wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu.
Wizara ya Mambo ya Ndani, kikiwa ndicho chombo cha kuendesha uchaguzi, ina jukumu na masuulia makubwa katika uga huo. Kwa hiyo, baada ya kutolewa agizo la kuanza shughuli za uchaguzi na wizara hiyo katika Makao Makuu ya shughuli za uchaguzi, huundwa tume ya uendeshaji wa uchaguzi ili kutayarisha taratibu za utangulizi kwa ajili ya kuendesha uchaguzi wa kisheria na wa haki.
Kwa upande mwingine, moja ya nukta muhimu katika uchaguzi wowote ule ni kuwachagua watu wenye sifa na wanaofaa zaidi kushika nyadhifa muhimu, nukta ambayo inalihusu Bunge pia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, aliigusia nukta hii muhimu jana asubuhi kabla ya kuanza darsa ya marhala ya juu kabisa ya Fiqhi aliposisitiza kwa kusema: Cheo chochote na uwezo wowote unaambatana na masuulia na jukumu maalumu. Inapasa ujitazame, je unao uwezo wa kutekeleza jukumu hilo au la? Hili ni somo kubwa sana.
Kuhusiana na suala hili kuna marekebisho kadhaa yamefanyika katika sheria ya uchaguzi wa Bunge, ili, mbali na kusahihisha baadhi ya kasoro, kuhakikisha watu wanaopitishwa kugombea nafasi za ubunge wana kiwango cha juu kabisa kinachotakiwa cha uwezo wa kiutaalamu, kielimu na kiuongozi.
Kwa muktadha huo, vigezo kadhaa vimewekwa ikiwemo kiwango cha juu cha elimu na kuwa na uzoefu wa miaka isiyopungua mitano ya tajiriba katika masuala ya utendaji, ikiwa ni sehemu ya masharti maalumu yanayopasa kutimizwa na wanaojiandikisha kwa ajili ya kutaka kugombea ubunge.
Moja ya mambo ya kujivunia kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuendesha chaguzi mbali mbali. Suala hili muhimu lilirasimishwa baada ya kupita miezi michache tu tangu ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kuitishwa kura ya maoni ya kuasisi Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu; na baada ya hapo zikaanza kufanyika chaguzi kadhaa zilizohusisha mirengo yenye mielekeo na mitazamo tofauti.
Katika kila uchaguzi uliofanyika nchini, ukiwa ndio utaratibu muhimu zaidi wa kuainisha mustakabali wa kisiasa wa nchi, wananchi wa Iran wamekuwa wakishiriki kwa uelewa, basira na uono mpana wa kisiasa; na daima wanaliangalia suala hilo kama jukumu na masuulia kwao.
Kwa kushiriki kwa wingi katika kila uchaguzi, wanananchi wa Iran wameonyesha kuwa, kama raia, wanaipa umuhimu na kuithamini haki ya kila mmoja wao kutumia kura yake kwa ajili ya kupitisha kwa busara maamuzi ya pamoja.
Kuendelea kwa utaratibu huu kunaonyesha kuwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu umejengeka kutokana na kura na chaguo la moja kwa moja; na uhalali wa kisiasa wa taasisi za utekelezaji na mihimili ya mfumo likiwemo Bunge vinatokana na kura na chaguo la wananchi.
Kwa hivyo kufanyika kwa nidhamu maalumu chaguzi za Rais, Bunge na Baraza la Wanazuoni wa Kumchagua Kiongozi Mkuu ni katika kuimarisha nguvu na uwezo wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Kwa mtazamo huo, kufanyika uchaguzi wa Bunge la 11, ambao ni wa kwanza katika awamu hii ya Hatua ya Pili ya Mapinduzi kunaufanya uchaguzi huo uwe na umuhimu wa maradufu.../