Mkuu mpya wa IAEA ataka uhusiano chanya na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i57651
Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesema ana matarajio makubwa kwamba taasisi hiyo itakuwa na uhusiano chanya na amilifu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Dec 03, 2019 07:51 UTC
  • Mkuu mpya wa IAEA ataka uhusiano chanya na Iran

Mkurugenzi Mkuu mpya wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA amesema ana matarajio makubwa kwamba taasisi hiyo itakuwa na uhusiano chanya na amilifu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 Rafael Mariano Grossi amesema kadhia ya Iran ni katika vipaumbele vya kwanza katika uongozi wake, huku akisisitiza kuwa ukaguzi utafanyika kwa uadilifu sio tu kwa Iran bali kwa nchi zote wanachama.

Amesema, "Ninataka kuihakikishia jamii ya kimataifa kuwa mimi ni mtu huru na nisiyesukumwa na mawimbi ya mashinikizo. Lengo langu ni kuifanya taasisi hii iwe ya uwajibikaji na uwazi zaidi."

Mwanadiplomasia huyo wa Argentina ni raia wa kwanza wa Amerika ya Latini kushika wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, tangu taasisi hiyo ya UN iundwe mwaka 1957.

Kwa upande wake, Kazem Gharib Abadi, Balozi na Mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA amesema Tehran inatumai pia kuwa, uhusiano wake na taasisi hiyo utakuwa chanya, na wakala huo utaendesha shughuli zake kwa njia huru na bila kuegemea upande wowote.

Kazem Gharib Abadi, Balozi na Mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA

Kadhalika amepongeza nafasi ya IAEA chini ya mkuu wake wa zamani, Yukia Amano, akisema kuwa wakala huo wa UN ulikuwa na nafasi muhimu katika kufikiwa na kulindwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Aidha ameikosoa Marekani kwa kujiondoa kwenye mapatano hayo ya kimataifa na kuiwekea vikwazo vya kidhalimu Jamhuri ya Kiislamu.

Katika ripoti zake ambazo tangu awali imekuwa ikizitoa kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA siku zote umekuwa ukitangaza wazi kwamba Iran imefungamana na kutekeleza kikamilifu majukumu yake.