Rouhani: Marekani ndio mzizi wa matatizo ya Waislamu duniani
(last modified Thu, 19 Dec 2019 04:08:00 GMT )
Dec 19, 2019 04:08 UTC
  • Rouhani: Marekani ndio mzizi wa matatizo ya Waislamu duniani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema uingiliaji mambo wa Marekani ndilo chimbuko la matatizo na migogoro inayoukabili uliwemwengu wa Kiislamu hii leo.

Rais Rouhani aliyasema hayo jana Jumatano mjini Kuala Lumpur, katika mazungumzo yake na Mahathir bin Mohamad, Waziri Mkuu wa Malaysia na kusisitiza kuwa, "Kuna udharura wa nchi za Kiislamu kuwa na ushirikiano ili ziweze kuyashinda mashinikizo ya madola makubwa hususan Marekani."

Amesema akthari ya matatizo yanayowakabili Waislamu hii leo yametokana na uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine unaofanywa na Marekani, vikiwemo vikwazo vya Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ameeleza bayana kuwa, vikwazo na mashinikizo hayawezi kulifanya taifa la Iran liache kuimarisha uhusiano wake na mataifa mengine, na kuongeza kuwa, "Kuna haja ya Tehran na Kuala Lumpur kuboresha uhusiano wao wa pande mbili katika nyuga mbalimbali zikiwemo sekta za sayansi, teknolojia, tiba, nishati, viwanda, utalii na teknolojia ya habari na mawasiliano."

Dakta Rouhani ambaye yuko mjini Kuala Lumpur Malaysia kushiriki katika kikao maalumu cha viongozi wa nchi za Kiislamu amebainisha kuwa, anatumai kuwa mkutano huo utakuja na suluhisho kwa matatizo yanayozikumba nchi za Kiislamu duniani, hususan nchi za Mashariki ya Kati.

Rais Rouhani na Dakta Mahathir wakiongoza jumbe zao kwenye mazungumzo jijini Kuala Lumpur

Kwa upande wake, Mahathir bin Mohamad, Waziri Mkuu wa Malaysia ambaye ni mwenyeji wa mkutano huo amesema, nchi yake ina hamu ya kuimarisha uhusiano na Iran katika nyuga mbalimbali na haswa uga wa biashara.

Dakta Mahathir bin Mohamad ameongeza kuwa, "Tutaendelea kuwa na uhusiano wa kibiashara na kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."

Amekariri kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni haramu na vinavyokanyaga miongozo ya Umoja wa Mataifa, huku akieleza bayana kuwa anatumai Tehran itaendelea kusimama kidete mkabala wa mashinikizo ya Marekani na Ulaya.