Kiongozi Muadhamu: Watu wa eneo hili wanaichukia sana Marekani
Kiongozi Muadhamu wa Mapinzudi ya Kiislamu akibainisha kwamba, 'Mimi, serikali na taifa la Iran tunalaani vikali shambulizi la Marekani dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq', amesisitiza kuwa, watu wa eneo hili wanaichukia sana Marekani.
Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo leo alipokutana na maelfu ya wauguzi kutoka maeneo yote ya Iran, na kubainisha kwamba wimbi la kuchukiwa Marekani katika eneo hili hususan nchini Iraq, ni radiamali ya kawaida ya wananchi kutokana na jinai za Marekani. Ameongeza kwamba kwa hakika shambulizi la Marekani dhidi ya Hashdu sh-Sha'abi ya Iraq ni ulipizaji kisasi wa Marekani kwa kushindwa genge la kigaidi la Daesh (ISIS) kwani wanamuqawama hao wa Hashdu sh-Sha'abi ndio waliolitokomeza genge hilo. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei pia ameashiria matamshi ya rais wa Marekani ya kuitwisha lawama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa eti ni muhusika mkuu wa kadhia ya siku ya jana Jumanne nchini Iraq na vitisho vyake kwa taifa la Iran, na kusisitiza kwamba, Marekani imekosea kwa kuwa suala hilo halihusiani na Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa, wote wanapaswa kufahamu kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitaki vita, lakini mtu yeyote anayetishia maslahi, izza, adhama na maenendeleo ya taifa la Iran, atakabiliwa na kipigo kikali kutoka kwa nchi hii bila kuchelewa. Kadhalika Kiongozi Muadhamu ameashiria jinai za Marekani hususan kupitia idara khabithi ya 'Black Water' nchini Iraq na Afghanistan na pia mauaji ya maelfu ya wasomi wa Iraq na raia wa kawaida na kuongeza kuwa, safari ya viongozi wa Marekani katika baadhi ya nchi za eneo tena bila ya idhini ya nchi husika na kufikia katika ngome zao za kijeshi, ni ishara nyingine ya mienendo ya dharau ya Marekani dhidi ya nchi na mataifa ya eneo hili. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amebainisha kwamba taifa la Iran ni taifa shujaa, lenye mtazamo mpana na lililo na utayarifu katika nyuga zote na kwamba ushindi ni wa taifa la Iran. Amesisitiza kuwa mustakbali wa kesho wa nchi hii utakuwa bora zaidi kuliko ilivyo hivi sasa.