Iran yajibu uvumi unaoenezwa kuhusu chanzo cha ajali ya ndege ya Ukraine
Mkuu wa shirika la ndege la Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio yenye wajibu wa kuchunguza ajali ya ndege ya abiria aina ya Boing 737 ya Ukraine iliyoanguka katika anga ya mji wa Tehran.
Akizungumza katika mahojiano na kanali ya pili ya televisheni ya Iran Ali Abedzadeh ameeleza kwamba: Iran haioni uzito wowote kukabidhi kisanduku cheusi cha taarifa za ndege ya Boing 737 ya Ukraine.
Amefafanua kuwa: Marekani na shirika la ndege la Boing zimepata hasara kubwa katika miezi kadhaa ya karibuni; na kama itabainika kuwa kuanguka kwa ndege ya Ukraine katika anga ya Iran kumetokana na hitilafu za mitambo, bila shaka hisa za shirika la Boing zitaporomoka mno; kwa sababu hiyo zimeamua kueneza uvumi.
Mkuu wa shirika la ndege la Iran amesema, kuna sababu nyingi za kuonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kati ya kuanguka kwa ndege hiyo na mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran.
Abedzadeh amefafanua kwa kusema: Shirika la Kimataifa la Safari za Anga (ICAO) limeainisha uhusiano uliopo baina ya miundo na mifumo ya kijeshi na ya ndege za kiraia kwa nchi zote; na uhusiano wa shirika la ndege la Iran na miundo yake ya kijeshi unafuata kanuni za Shirika la Kimataifa la Safari za Anga.
Amesema mashuhuda waliiona ndege hiyo imeshika moto ulioendelea kuwaka kwa muda wa dakika nzima, ambapo kama ndege hiyo ingekuwa imetunguliwa na kombora ingeripuka bila kupita muda.
Aidha amekanusha madai ya kupatikana mabaki ya kombora kando ya ndege hiyo iliyoanguka na kueleza kwamba, mripuko uliotokea umesababishwa na mgongano wa ndege hiyo na ardhi wakati wa kuanguka.
Jana Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau, baadhi ya maafisa wa Marekani na baadhi ya vyombo vya habari vya kigeni vilidai kuhusu chanzo cha ajali ya ndege ya abiria ya Ukraine iliyoanguka katika anga ya Tehran kwamba, yumkini ndege hiyo ilitunguliwa na kombora la Iran bila kukusudia.
Jumatano asubuhi, ndege moja ya abiria ya shirika la ndege la Ukraine aina ya Boing 737 ilianguka karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Imam Khomeini mjini Tehran, ambapo abiria wote 167 pamoja na wahudumu 9 waliokuwemo ndani yake walifariki dunia.../