Rais Rouhani: Wananchi wa Asia Magharibi wahakikishe Marekani inaondoka katika eneo
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, kuna udharura kwa wananchi wa Asia Magharibi kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, majeshi ya Marekani yanaondoka katika eneo hili.
Rais Rouhani amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika kikao na baraza lake la mawaziri ambapo amemtaja shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani kuwa alikuwa mlinzi wa mipaka ya Iran.
Rais Rouhani ameashiria kuuawa shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani na kueleza kwamba, kuuawa kwake kulikuwa kwa kidhulma, watu waliopoteza maisha yao pia katika msongamano huko Kerman na watu waliofariki dunia katika tukio la kuanguka ndege ya abiria ya Ukraine yote hayo ni matukio ambayo yaliwasha moto wa huzuni katika nyoyo za watu na kuleta maumivu makubwa.
Sambamba na kueleza udharura wa wananchi wa Asia Magharibi kufanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba, majeshi ya Marekani yanafukuzwa katika eneo hili, Rais Rouhani amesema kuwa, tukio la kudunguliwa kimakosa ndege ya abiri ya Ukraine liliwaumiza watu wote.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taasisi za serikali zinashiriki katika uchunguzi wa kuanguka ndege ya Ukraine kwani haiwezekani kulifumbua macho kosa hili ambalo linaumiza mno.
Kuhusiana na kadhia ya nyuklia, Rais Hassan Rouhani amesema kuwa, miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika kwa usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na haya madai kwamba, eti Tehran inataka kutengeneza silaha za nyuklia ni ya kijinga na yasiyo na msingi wowote.