Iran yaionya Marekani kwa kutoa madai 'hatari' dhidi yake
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i59719-iran_yaionya_marekani_kwa_kutoa_madai_'hatari'_dhidi_yake
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inapaswa kuangali upya uwepo wa vikosi vyake vamizi katika eneo la Asia Magharibi badala ya kuibua tuhuma zisizo na msingi wowote dhidi ya mataifa mengine.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 13, 2020 12:52 UTC
  • Sayyid Abbas Mousavi
    Sayyid Abbas Mousavi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Marekani inapaswa kuangali upya uwepo wa vikosi vyake vamizi katika eneo la Asia Magharibi badala ya kuibua tuhuma zisizo na msingi wowote dhidi ya mataifa mengine.

Sayyid Abbas Mousavi amesema hayo Ijumaa ya leo ambapo pia amemkosoa vikali Rais Donald Trump wa Marekani kwa kuituhumu Iran kuwa imehusika na shambulizi la hivi karibuni dhidi ya kambi ya jeshi vamizi la Marekani nchini Iraq.

Wizara ya Ulinzi wa Marekani imetangaza kuwa ndege zake za kivita zimeshambulia maeneo matano ya Brigedi za Hizbullah ya Iraq. Kwa mujibu wa Pentagon, sehemu kubwa ya maeneo hayo yaliyolengwa yalikuwa maghala ya silaha za harakati hiyo ya Muqawama.

Trump ametoa amri ya kutekelezwa hujuma hizo kwa madai kuwa, askari wawili wa nchi hiyo na mwengine mmoja wa Uingereza wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi la maroketi lililofanywa dhidi ya kambi ya kijeshi ya Taji katika mkoa wa Salah ad Din wa kaskazini mwa Baghdad, mji mkuu wa Iraq. 

Wanajeshi vamizi wa US nchini Iraq

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameeleza bayana kuwa, "badala ya kuchukua hatua za hatari na kuibua madai yasiyo na msingi, Trump anapaswa kutizama upya mienendo ya vikosi vyake katika eneo hili."

Sayyid Mousavi ameongeza kuwa, Marekani haipaswi kuzilaumu nchi nyingine kwa hatua zinazochukuliwa na wananchi wa Iraq za kulipiza kisasi cha kuuawa makamanda na askari wao na wanajeshi vamizi.