Mar 16, 2020 02:34 UTC
  • Zarif aitaka dunia izuie ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya Iran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewaandikia barua mawaziri wenzake wa mambo ya nje wa nchi mbali mbali duniani, akiwaomba wazuie na kukomesha ugaidi wa kiuchumi wa Marekani dhidi ya taifa hili.

Katika barua hiyo, Mohammad Javad Zarif ametilia mkazo ulazima wa kuondolewa vikwazo vyote vya upande mmoja, haramu na visivyo vya kisheria vya Marekani dhidi ya Iran ili kuweza kukabiliana na maradhi ya Corona.

Nakala za barua hiyo zimekabidhiwa mabalozi na wanadiplomasia wa nchi mbali mbali hapa nchini jana Jumapili, na wasaidizi wa Dakta Zarif.

Dakta Zarif kwenye barua hiyo amekosoa kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa ugaidi wa kiuchumi wa Washington dhidi ya Iran, ambao umekuwa na taathira hasi hususan katika sekta ya afya hapa nchini.

Kufikia sasa watu 13,989 wameambukizwa Corona nchini Iran; 4790 miongoni mwao wamepona huku wengine 724 wakipoteza maisha

Wiki iliyopita pia, Zarif alimwandikia barua Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akisisitiza ulazima wa kuondolewa vikwazo hivyo haramu vya upande mmoja ilivyowekewa Iran na Marekani.

Hivi karibuni, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema Rais Donald Trump ameshadidisha vikwazo haramu vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Iran kwa lengo la kufyonza rasilimali za taifa hili zinazohitajika kwa ajili ya kupambana na virusi hatari vya Corona; na kusisitiza kuwa ugaidi wa kiuchumi wa Marekani hivi sasa umegeuka na kuwa ugaidi wa kimatibabu.

Tags