Trump akariri tena ombi lake la kufanya mazungumzo na Iran
Rais Donald Trump wa Marekani amedai kwamba, 'Marekani haitaki uadui na Iran na kwamba italazimika kufanya nayo mazungumzo.'
Ameyasema hayo katika mwendelezo wa matamshi yake katika kikao na waandishi wa habari ndani ya ikulu ya White House kuhusu muda wa kufutwa vikwazo dhidi ya Iran ambapo amesema: "Tazameni, tunatakiwa kuzungumza nao. Ninadhani tunaweza kufikia haraka sana makubaliano na Iran. Kazi tu wanayotakiwa kuifanya ni kutupigia simu." Aidha Trump ameongeza kwamba: "Ninadhani wao ni watu wenye majivuno na uongozi wao pia ni wenye majivuno, kama tulivyo sisi sote, watu wetu na sisi pia ni wenye majivuno. Ni vigumu wao kutupigia simu na ni vigumu wao kuandaa mazungumzo. Lakini wanaweza kutatua matatizo ya nchi yao kirahisi sana."
Akiendelea, rais huyo wa Marekani amedai kwa kusema: "Hatutaki uadui, lakini wao wanatufanyia uadui na kwa hilo watajuta kiasi ambacho hawajawahi kukishuhudia." Matamshi ya Trump yanatolewa wakati ambao serikali ya Washington na baada ya kujiondoa kinyume cha sheria kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA hapo tarehe 8 Mei 2018, imeiwekea Iran vikwazo na mashinikizo ya juu kabisa. Katika upande wa pili, viongozi wa Iran wamesisitiza kuwa watazungumza na Marekani iwapo tu serikali ya Washington itaachana na siasa zake za uhasama dhidi ya Tehran na kisha kurejea kwenye mapatano hayo katika fremu ya mazungumzo ya kundi la 5+1.