Iran yazindua mfumo mpya wa kupima COVID-19
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua mfumo mpya wa kupima ugonjwa wa COVID-19 au corona. Mfumo huo unatumia Akili Bandia au Artificial Intelligence na unatumia taswira za mashine ya CT Scan kubainisha kuwepo ugonjwa wa corona katika mwili wa binadamu.
Mfumo huo ambao umeundwa na watafiti wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Shariff umezinduliwa Jumamosi mjini Tehran katika sherehe ambayo imehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Iran anayeshughulikia masuala ya sayansi na teknolojia Dkt. Sorena Sattari. Akizungumza katika uzinduzi huo, Dkt. Sattari amesema mfumo huo uliozinduliwa unatoa matokeo bora zaidi kuliko kile kifaa cha kawaida cha kupima corona.
Naye Dakta Hamid-Reza Rabiee, Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Sayansi na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Shariff amesema kupiga picha kifua kwa kutumia CT Scan ni njia bora zaidi ya kubaini iwapo mtu ameambukizwa corona au la. Amesema hivi sasa duniani ni Marekani na China pekee ndizo zina mfumo sawa na huo wa Iran wa kupima corona. Amesema watafiti vijana wa Iran wamefanikiwa kuunda mfumo huo wa kisasa wa kupima corona.
Aidha Dakta Rabiee amesema vifaa vya sasa vya kupima corona duniani vina kasoro nyingi na kuongeza kuwa: "Mfumo uliozinduliwa leo na Iran una uwezo wa hadi asilimia 97 wa kufanya uchunguzi bila makosa." Aidha amesema mfumo huo utaanza kutumiwa rasmi wiki ijayo katika hospitali na vituo vya tiba nchini.
Naye Dkt. Ali Reza Zalii, Mkuu wa Idara ya Kukabiliana na Corona mjini Tehran amesema mashine ya CT Scan ni njia bora zaidi ya kupima corona kwa watu wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa huo. Ameongeza kuwa: "Mfumo huu wa kupima corona nchini Iran ni bora kuliko mifumo mingine duniani."
Wiki kadhaa zilizopita pia Iran ilianza kutengeneza kwa wingi kifaa cha kupima corona na sasa imejitosheleza katika uga huo na haihitajii msaada wa kigeni.