Iran: Tunatumia mbinu mpya kutambua waathiriwa wa corona
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60473-iran_tunatumia_mbinu_mpya_kutambua_waathiriwa_wa_corona
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vipimo vinavyofanywa vya proteini mpya ijulikanayo kiutalamu kwa jina la "fungomwili" au antibody ni miongoni mwa mbinu mpya zinazotumiwa na Iran kutambua wagonjwa wa COVID-19.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2020 10:30 UTC
  • Iran: Tunatumia mbinu mpya kutambua waathiriwa wa corona

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, vipimo vinavyofanywa vya proteini mpya ijulikanayo kiutalamu kwa jina la "fungomwili" au antibody ni miongoni mwa mbinu mpya zinazotumiwa na Iran kutambua wagonjwa wa COVID-19.

Rais Rouhani amesema hayo leo Jumapili katika kikao cha Kamati ya Taifa ya Kupambana na Kirusi cha Corona na kuongeza kuwa, kila pale watu wanapogunduliwa kuambukizwa kirusi cha corona, kazi ya kuwachunguza watu waliokuwa na mawasiliano nao huanza mara moja ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha kwamba taarifa sahihi na za kina zinapatikana kuhusu maambukizi ya COVID-19.

Vile vile amegusia data na takwimu zinazotolewa na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Kirusi cha Corona kutoka vituo vyote nchini Iran na kusisitiza kuwa, takwimu hizo zinaonesha kuwa ugonjwa wa corona umekaribia kudhibitiwa humu nchini.

Rais Rouhani amezungumzia pia aplikesheni (application) iliyobuniwa na Chuo Kikuu cha Sharif hapa Iran cha kufanya uchunguzi wa corona na kusema kuwa, kwa mujibu wa aplikesheni hiyo na data zinazotolewa na Wizara ya Afya ya Iran tunaweza kutambua ni mtu gani ana hali mbaya yaani rangi nyekundu na nani ana hali ya kutia shaka yaani rangi ya njano ambao wote hao lazima wafuatiliwe na hatua za haraka zichukuliwe juu yao.

Vifaa vipya vya kupambana na corona nchini Iran

Hayo yanajiri katika hali ambayo, tayari Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua na kuonesha hadharani bidhaa mbali mbali za kiteknolojia za kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19 yaani corona ambazo zimeundwa na mashirika ya elimu-msingi ya Iran ambayo msingi wake ni elimu kwa kimombo knowledge-based companies.

Miongoni mwa bidhaa hizo ni kifaa cha kupima haraka corona, kifaa cha ozonizer, lango  maalumu lenye uwezo wa kupulizia dawa za kuua virusi kwenye magari yanayopita na pia kugundua kiwango cha joto kwa waliomo ndani ya gari, aplikesheni ya Tak inayohusu lishe  na kinga ya corona pamoja na kifaa chenye uwezo wa kugundua mwili na sehemu kilipo kirusi cha corona katika umbali wa mita 100 tena katika kipindi cha sekunde chache tu. Kifaa hicho ambacho ni mara ya kwanza kabisa kuvumbuliwa duniani kimepewa jina la "Musta'an 110," na kinaweza kugundua corona bila ya kuchukua vipimo vya damu. Sherehe za uzinduzi wa kifaa hicho cha kipekee zilihudhuriwa na Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH  jeshi ambalo liko mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya corona nchini Iran.