Zaidi ya wagonjwa 77 elfu wa COVID-19 wamepona nchini Iran
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa 77 elfu na 350 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran alitangaza hayo jana Jumamosi na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 802 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia jana adhuhuri watu 96,448 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.
Daktari Jahanpur amezungumzia pia kufariki dunia wagonjwa 65 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,156 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.
Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran amesema kati ya wale wote walioambukizwa corona nchini Iran, asilimia 80 wameweza kutibiwa na kupataa nafuu na hivyo kuruhusiwa kuondoka hospitalini.
Idadi ya walioambukizwa corona duniani kote ni takribani milioni 3.5 ambapo watu wasiopungua 240,000 wameaga dunia na wengine zaidi ya milioni moja wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.