Rouhani aitaka EU iishinikize Israel isitishe mashambulizi yake Syria
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili linataraji kuwa Umoja wa Ulaya utaushinikiza utawala haramu wa Israel ukomeshe mashambulizi yake dhidi ya Syria.
Rais Rouhani alisema hayo jana Jumatano katika mazungumzo yake ya simu na mwenzake wa Austria, Alexander Van der Bellen na kueleza bayana kuwa, "Iran ya Kiislamu inafuatilia amani na uthabiti katika eneo, na Ulaya inatarajiwa kuushinikiza utawala wa Kizayuni na isiuruhusu uendeleze mashambulizi yake dhidi ya Syria na Lebanon, pamoja na Ukanda wa Gaza ulio chini ya mzingiro, katika kipindi hiki cha janga la corona."
Hivi karibuni, raia kadhaa wa Syria waliuawa na kujeruhiwa katika shambulio la makombora lililofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya maeneo ya makazi ya raia katika vitongoji vya al-Hajirah na al-Adilah kandokando ya Damascus, mji mkuu wa Syria; huo ukiwa ni muendelezo wa mashambulio unaoyafanya kila baada ya muda dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Kadhalika Dakta Rais Rouhani ameashiria kuhusu njama za Marekani za kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusisitiza kuwa, Tehran katu haitakubali ukiukwaji wowote wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema, "tunaamini kuwa, Umoja wa Ulaya unapaswa kuchukua hatua zaidi za kivitendo ili kuonyesha mfungamano wake na masuala ya kimataifa na makubaliano ya JCPOA."

Aidha Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia juu ya janga la kimataifa la corona na kubainisha kuwa, vikwazo vya Marekani vinakwamisha jitihada za pamoja za dunia za kuushinda ugonjwa wa Covid-19 ambao umeua malaki ya watu, mbali na mamilioni kukumbwa nao.
Kwa upande wake, Rais Alexander Van der Bellen mbali na kueleza juu ya utayarifu wa nchi yake wa kuimarisha ushirikiano na Iran amesema Austria na Umoja wa Ulaya kwa ujumla zinapinga vikwazo vya upande mmoja vya Washington dhidi ya Iran na kwamba EU itaendelea kushirikiana na Tehran licha ya vikwazo hivyo.