Kiongozi Muadhamu atilia mkazo udharura wa kujifunza fikra za hayati Imam Khomeini
(last modified Thu, 04 Jun 2020 07:39:54 GMT )
Jun 04, 2020 07:39 UTC
  • Kiongozi Muadhamu atilia mkazo udharura wa kujifunza fikra za hayati Imam Khomeini

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema jana alihutubia taifa kwa njia ya televisheni kwa mnasaba wa kukumbuka siku aliyoaga dunia hayati Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akisema kuwa kutaka mabadiliko, kuwa na ari ya kufanya mabadiliko na kuyafanya mageuzi ni miongoni mwa sifa muhimu za hayati Imam Khomeini.

Ayatullah Khamenei amemtaja Imam Khomeini kuwa ni "Imamu na kinara wa mageuzi" na kusema: Ili kubakisha hai Mapinduzi ya Kiislamu tunalazimika kujifunza sifa hii ya hayati Imam, kuwa na mwelekeo wa mageuzi na mtazamo wa kuwa bora zaidi na kwa kasi na vilevile harakati ya kusonga mbele katika medani zote hususan katika nyanja ambazo hazikupiga hatua au ambazo zimerudi nyuma. 

Imam Ruhullah Khomeini alikuwa mwanamapambano na mwanafikra angavu aliyeyajua vyema masuala ya Iran na Ulimwengu wa Kiislamu; kwa msingi huo njia aliyotumia katika kupambana na ubeberu na tawala za dhalimu ni njia ya kudumu na isiyo na mwisho. 

Imam Khomeini

Katika hotuba yake ya jana Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria moja kati ya matunda muhimu ya mtazamo wa kupenda mageuzi wa hayati Imam Khomeini na kutaja kusimama kwake imara na kuyadhalilisha madola makubwa ya kibeberu. Alisema: Wakati fulani hakuna mtu aliyekuwa akithubutu hata kujibizana na Marekani, lakini Imam Khomeini alifanya mageuzi katika mtazamo wa watu kuhusiana na madola makubwa, akayadhalilisha na kuthibitisha kwamba, madhalimu wa kimataifa wanaweza kupewa kichapo; na uhakika huu ulishuhudiwa katika kusambaratika Urusi ya zamani na unashuhudiwa hii leo kuhusiana na Marekani.

Kwa upande huu inatupasa kusema kuwa, fikra za kisiasa za hayati Imam Khomeini zilikuwa mwanzo wa mabadiliko adhimu ambayo yaliweza kuyafundisha mataifa mbalimbali uwezo mkubwa wa kisiasa wa Uislamu kama injini madhubuti ya watu wanaotaka kufanya mageuzi na mabadiliko. 

Hapana shaka yoyote kwamba, njia ya kumkomboa mwanadamu kutoka kwenye minyororo ya dhulma na ubaguzi wa tawala za kibeberu ni wanadamu wenyewe kuijua haki na hakika. Kinachojiri sasa katika jamii ya Marekani ni mfano wa wazi katika uwanja huu.

Hayati Imam Ruhullah Khomeini

Ayatullah Ali Khamenei ameyataja matukio ya sasa huko Marekani kuwa ni kudhihirika wazi uhakika uliokuwa umefichwa wa Marekani na kuongeza kuwa: Si jambo jipya kuona polisi wa Marekani akiweka goti lake juu ya shingo ya raia mweusi na kumbinya hadi kufa huku polisi wengine kadhaa wakitazama tu kwa macho mandhari hiyo. Haya ndiyo maadili na tabia ile ile ya serikali ya Marekani mambo ambayo Wamarekani wamekuwa wakiyafanya katika nchi nyingi za dunia kama Afghanistan, Iraq, Syria na kabla yake huko Vietnam.

Ayatullah Khamenei amesema nara na kauli mbiu inayotolewa na Wamarekani hii leo ambayo ni 'hatuwezi kupumua' ni kauli ya mataifa yote yanayodhulumiwa na kuongeza kuwa: "Marekani imefedheheka duniani kutokana na mienendo yake. Kuanzia usimamizi mbaya katika kupambana na ugonjwa wa corona ambako kutokana na ufisadi uliokita mizizi katika utawala wa Marekani, umesababisha maafa na idadi kubwa zaidi ya wagonjwa kuliko nchi nyingine na sasa mienendo hii miovu na jinai wanazofanya dhidi ya raia bila hata kuomba radhi na baadaye wanadai kuwa wanatetea haki za binadamu, kama kwamba bwana yule mweusi aliyeuawa  hakuwa mwanadamu wala hakuwa na haki ya aina yoyote."

Polisi wa Marekani wakimuua George Floyd

Ukweli huu pamoja na darsa ya kudumu inayopatikana katika fikra za Imam Khomeini vinaonyesha kuwa, japokuwa shughuli ya kukumbuka miaka 31 tangu Imam afariki dunia imefanyika katika mazingira makhsusi kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, lakini bado inatoa ujumbe na darsa nyingi zinazopaswa kusomwa vyema na kutumiwa na wanadamu wanaopigania haki na uadilifu kote duniani.  

Tags