Meja Jenerali Salami: Nembo za dola kubwa la Marekani zameanza kuporomoka
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema mienendo ya nchi za dunia inabadilika na kuongeza kuwa: "Nembo zote ambazo Marekani imekuwa ikizitumia kujiarifisha kama dola kubwa duniani na kuzitumia kuwasilisha taswira isiyo ya kweli sasa zimeanza kusambaratika."
Meja Jenerali Hussein Salami Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameyasema hayo leo Jumatano na kuashiria uwezekano wa kusambaratika mapema kabla ya wakati na kwa kasi maadui wa Iran, hasa Marekani na kuongeza kuwa Marekani imekuwa ikiwasilisha taswira ambayo inaionyesha kuwa ni nchi maridadi iliyostawi lakini ukweli mchafu ambao ulikuwa umejificha kuhusu nchi hiyo sasa unazidi kubainika.
Salami ameongeza kuwa: "Marekani imekuwa ikijinadi kuwa kitovu cha uhuru na haki za binadamu duniani lakini nembo hizo sasa zimeporomoka."
Kamanda Mkuu wa IRGC ameongeza kuwa, hatua ya meli za mafuta za Iran kufikisha mafuta Venezuela kutoka Ghuba ya Uajemi ni ishara ya irada na zoezi la kuonyesha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesema leo Iran iko katika kilele cha nguvu na izza na kwamba inaendelea kuvuka matatizo inayokumbana nayo.
Hivi karibuni, meli hizo tano za Iran zilifanikiwa kutia nanga nchini Venezuela pamoja na kuwepo vitisho vya Marekani vya kutumia nguvu za kijeshi kuzuia meli hizo kufika Venezuela.
Kufuatia vitisho hivyo vya Marekani, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitahadharisha kuhusu chokochoko za Marekani katika Bahari ya Caribbean na kusema: "Iwapo meli za mafuta za Iran zitasumbuliwa na Wamarekani popote pale duniani, basi Iran nayo itawaibulia matatizo."
Meli tano za Iran zimefikisha bidhaa za mafuta kwa mafanikio nchini Venezeula na sasa ziko njiani zikirejea nyumbani.