Rouhani: Uhuru wa kujitawala na usalama wa Iran na Iraq vinafungamana
Rais Hassan Rouhani wa Iran na Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi wamesema uhusiano wa Tehran an Baghdad unavuka mipaka ya nchi mbili hizi jirani, na kusisitiza kuwa: Uhuru wa kujitawala na usalama wa Iran na Iraq vina mfungamano mkubwa.
Katika mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq jana Jumanne hapa mjini Tehran, Rais Hassan Rouhani alisema: Iran na Iraq zina mambo mengi ambayo yanazileta pamoja, kuanzia masuala ya utamaduni, dini, historia, na siasa. Amesema Hauza za kidini za mjini Qum nchini Iran na Najaf nchini Iraq ni hazina kubwa na yenye manufaa kwa mataifa haya mawili ya Kiislamu.
Rais Rouhani ameeleza bayana kuwa, usalama na amani ya Iraq ina umuhimu mkubwa kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na kwamba majeshi ajinabi yameshindwa kuvuruga uhusiano wa kidugu uliopo baina ya nchi mbili hizi jirani.
Dakta Rouhani amesema Iran inaunga mkono nafasi ya Iraq kama dola lenye nguvu la Kiislamu na Kiarabu, katika kuhakikisha kuwa amani na uthabiti unashuhudiwa katika eneo la Asia Magharibi. Amesema nchi mbili hizi zinapania kunyanyua kiwango cha mabadilishano yao ya kibiashara hadi dola bilioni 20.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Iraq, Mustafa al-Kadhimi ambaye aliwasili jana Jumanne hapa nchini kwa safari rasmi ya kikazi, amesisitizia umuhimu wa kuimarishwa na kufikishwa katika kiwango cha juu zaidi uhusiano baina ya Tehran na Baghdad katika nyuga mbalimbali.
Ameongeza kuwa, katika mazungumzo yake na Rais Rouhani, imeafikiwa suala la kuundwa Kamati ya Pamoja ya kufuatilia na kuharakisha utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya nchi mbili hizi.