Dakta Muhammad Javad Zarif: Saudi Arabia haitaki uhusiano ulio sawa na Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran iko tayari kuwa na uhusiano mzuri na Saudi Arabia, lakini inasikitisha kuwa, serikali ya Riyadh haitaki kuweko uhusiano ulio sawa baina yake na Iran.
Dakta Muhammad Javad Zarif amesema hayo mjini Moscow katika mkutano wake na waandishi wa habari akiwa na mwenyeji wake Sergei Lavrov, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Russia ambapo amebainisha kwamba, siku zote Tehran imekuwa ikitaka iwe na uhusiano mwema na mzuri na majirani zake.
Dakta Zarif ameeleza bayana kwamba, suala la kuweko uhusiano mzuri na mataifa jirani ni miongoni mwa sera zinazopewa kipaumbele na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kuwa, Iran ina azma na nia ya dhati ya kupanua ushirikiano wake na mataifa jirani yakiwemo yaliyoko katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kwamba, inatangaza wazi utayari wake wa kuwa na uhusiano na Saudia na Imarati ambao utakuwa umejengeka katika misingi ya kuheshimiana pande mbili.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria mpango wa usalama wa Russia kwa ajili ya Ghuba ya Uajemi na kukumbusha kwamba, Tehran imewahi kupendekeza pia mpango wa "Ubunifu wa Amani ya Hormuz" ambao kimsingi una lengo moja.
Aidha amesema pia kuwa, Iraq nayo inataka kuwa na ushirikiano katika kudhamini usalama wa Asia Magharibi na kueleza kwamba, Baghdad inaweza kuwa na mchango mkubwa katika kudhamini uthabiti na usalama wa eneo hili.