Jenerali Amir Hatami: Ushirikiano wa kijeshi wa Iran na Russia ni chanya
-
Brigedia Jenerali Amir Hatami
Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Russia ni chanya na unaoendelea kuimarika.
Brigedia Jenerali Amir Hatami alisema hayo jana Jumamosi baada ya kuwasili mjini Moscow, akiongoza ujumbe wa ngazi ya juu wa kijeshi na kiulinzi wa Iran na kuongeza kuwa, "tumeshuhudia ustawi mkubwa wa ushirikiano wa pande mbili, ingawaje mwaka huu umetatizwa kidogo na janga la corona."
Ameashiria luteka ya pamoja ya kijeshi kati ya Iran, Russia na China iliyofanyika hivi karibuni kaskazini mwa Bahari ya Hindi na Bahari ya Oman na kusisitiza kuwa, huo ni mfano hai wa kuendelea kuimarika ushirikiano huo.
Brigedia Jenerali Hatami amesema katika safari yake hiyo ya Moscow, anatazamiwa kushiriki warsha na maonyesho ya kijeshi ili kufuatilia kwa karibu mafanikio mapya katika uga wa kijeshi sambamba na kuzungumzia uhusiano wa pande mbili na masuala ya kieneo.
Aidha Waziri wa Ulinzi wa Iran anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na mwenzake wa Russia, Sergey Shoygu na maafisa wengine wa ngazi za juu wa nchi hiyo.
Kongamano na Maonyesho ya Kiufundi ya Kijeshi ya Russia hufanyika kila mwaka tokea mwaka 2015 kwa amri ya Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo, ambapo mafanikio mapya ya jeshi la Russia na sekta ya ulinzi ya nchi hiyo huonyeshwa.