Rais Rouhani: Leo Dunia ina imani na Iran na ahadi inazotoa
Rais Hassan Rouhani amesema leo dunia ina imani na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ahadi inazotoa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa Maonesho ya 29 ya Kimataifa ya Vitabu Tehran. Mbali na kuashiria kwamba kutokana na misingi ya itikadi zake Iran itaendelea kuheshimu ahadi zake, Rais Rouhani amesema safari za marais wa nchi mbalimbali hapa nchini na mikataba ya muda mrefu inayosainiwa inamaanisha imani iliyopo juu ya Iran.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa katika mazungumzo magumu na tata ya nyuklia taifa la Iran limepata mafanikio makubwa ambayo ni kwa manufaa ya Iran, upande wa pili kwenye mazungumzo, eneo la Mashariki ya Kati na ulimwengu kwa jumla.
Rais Rouhani amesema matokeo ya mazungumzo ya nyuklia yalikuwa ni ya ushindi kwa pande zote mbili na kuongeza kuwa ukiondoa nchi moja au mbili katika eneo ambazo zinahisi zimepata hasara, makubaliano ya nyuklia yamezinufaisha nchi 188 duniani. Amefafanua kuwa baadhi ya nchi katika eneo zimekasirishwa na matokeo na mafanikio yaliyopatikana katika makubaliano ya nyuklia na hivyo zinajaribu kukwamisha utekelezaji wake.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ameyapongeza mashirika ya vitabu yaliyopata tuzo pamoja na wawakilishi wa nchi za kigeni waliohudhuria Maonesho ya 29 ya Kimataifa ya Vitabu Tehran hususan mwakilishi wa Rais wa Russia.
Maonesho ya 29 ya Kimataifa ya Vitabu Tehran yamefunguliwa rasmi leo kwa kauli mbiu ya "Utakuwa Umechelewa Ukisoma Kesho." Maonesho hayo yataendelea hadi tarehe 14 mwezi huu wa Mei.../