Sep 20, 2020 02:39 UTC
  • Ulyanov: Jamii ya kimataifa imepuuza madai ya Marekani dhidi ya Iran

Mwakilishi wa Russia katika jumuiya za kimataifa mjini Vienna ameunga mkono barua iliyotumwa na Troika ya Ulaya katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu suala la kusitishwa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran na kusema jitihada zinazofanywa na Marekani kwa ajili ya kurefusha muda wa vikwazo hivyo hazina mashiko wala mantiki.

Mikhail Ulyanov ambaye alikuwa akizungumzia tangazo la nchi tatu za Troika ya Ulaya, yaani Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kuhusu kuendelea kusitishwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran baada ya leo tarehe 20 Septemba, amesema madai ya Marekani ya kutaka kurefushwa muda wa vikwazo hivyo hayana maana wala mashiko. 

Ulyanov amesema kuwa, hakuna haja ya kutoa matamshi ya aina yoyote, kwa sababu jitihada za Marekani za kutaka kuhuisha vikwazo hivyo kwa kutumia utaratibu wa "Snapback Mechanism" hazina mashiko ya kisheria wala hadhi yoyote. 

Nchi tatu za Ulaya za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa ambazo ni maarufu kwa jina la Troika ya Ulaya kwa mara nyingine zimepinga njama za Marekani za kutaka kuirejeshea Iran vikwazo vilivyoondolewa na Umoja wa Mataifa baada ya kufikiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika barua yao ya Ijumaa iliyopita kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, nchi hizo tatu za Ulaya zilisisitiza kwamba kusimamishwa vikwazo vya Iran kutaendelea hata baada ya tarehe 20 Septemba na kwamba uamuzi au hatua yoyote ya kuirejeshea vikwazo Iran ni kinyume cha sheria.

Donald Trump

Katika barua yao hiyo, nchi za Uingereza, Ujerumani na Ufaransa kwa mara nyingine zimesisitiza kuwa zitaendelea kuheshimu mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Baada ya kushindwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Marekani imedai kuwa itavirejesha yenyewe vikwazo vya umoja huo dhidi ya Iran licha ya kwamba si mwanachama tena wa JCPOA. 

Tags