Zarif: Vikwazo vya Marekani ni kielelezo cha "ugaidi wa kitiba"
-
Muhammad Javad Zarif
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezungumzia athari mbaya za vikwazo vya Marekani katika shughuli za Iran za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona na kusema kuwa hatua hizo za Washington ni kielelezo cha ugaidi katika masuala ya tiba.
Muhammad Javad Zarif ambaye jana alikuwa akizungumza na televisheni ya Russia Today amekadhibisha madai ya Marekani inayosema kuwa haijaiwekea Iran vikwazo katika sekta ya masuala ya kibinadamu na kusema: Njama za Marekani za kuzuia uuzaji wa mafuta ya Iran katika masoko ya kimataifa zinakwamisha na kubana uwezo wa Tehran wa kukabiliana na maambukizi ya corona. Zarif ameashiria kasi ya maambukizi ya virusi vya corona na udharura wa kuwepo ushirikiano baina ya nchi zote kwa ajili ya kukabiliana na janga hilo na kusema: Marekani inabana vyanzo vya fedha vya Iran kwa kuzuia uuzaji nje mafuta ya nchi hii na imekuwa ikikwamisha jitihada zote za kurejesha nchini fedha za Iran zilizoko nje ya nchi.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema kuwa Marekani inazuia hata kutumwa fedha za Iran kwa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa ajili ya kununua chanjo ya COVID-19 na chanjo ya homa ya mafua (influenza).
Kuhusu mapatano ya karibuni baina ya Imarati na Bahrain na utawala haramu wa Israel, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran amesema: Kumekuwepo uhusianio wa siri baina ya Imarati na utawala haramu wa Israel kwa miaka mingi na uhusiano huo umetangazwa na kuwekwa wazi katika kipindi cha sasa ili kumsaidia Donald Trump katika kampeni za uchaguzi wa rais huko Marekani.