Kamanda Sharif: Viongozi vibaraka wa Kiarabu wamethibitisha ukibaraka wao kwa Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63689-kamanda_sharif_viongozi_vibaraka_wa_kiarabu_wamethibitisha_ukibaraka_wao_kwa_wazayuni
Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amezungumzia hatua ya nchi mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain ya kutangaza uhusiano wao wa kawaida wa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, viongozi wa nchi hizo wamethibitisha kivitendo ukibaraka wao kwa Wazayuni.
(last modified 2026-05-20T03:07:53+00:00 )
Sep 28, 2020 04:21 UTC
  • Kamanda Sharif: Viongozi vibaraka wa Kiarabu wamethibitisha ukibaraka wao kwa Wazayuni

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amezungumzia hatua ya nchi mbili za Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na Bahrain ya kutangaza uhusiano wao wa kawaida wa utawala wa Kizayuni na kusema kuwa, viongozi wa nchi hizo wamethibitisha kivitendo ukibaraka wao kwa Wazayuni.

Brigedia Jenerali Ramezan Sharif amesema hayo usiku wa kuamkia leo Jumatatu na kuongeza kuwa, watawala vibaraka wa nchi za Kiarabu za eneo hili wanadhani kwamba kama watajiegemeza kwenye nguzo zilizochakaa za utawala wa Kizayuni wataendelea na tawala zao lakini wajue kuwa hatua yao hiyo itawaletea majuto tu.

Amesema, hatua ya Imarati na Bahrain ya kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni haina matunda mengine isipokuwa hasira za Waislamu na kuzidi kujivua nguo watawala wa nchi hizo.

Baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu wanavyojipendekeza kwa mabeberu wa dunia

 

Msemaji wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH amewaambia watawala wa nchi za Kiarabu za eneo hili kwamba, kutumia vibaya upole wa nchi kubwa na yenye nguvu ya Iran katika suala hilo kuna mipaka na kama hawatosikiliza nasaha za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, basi majuto ndiyo yatakuwa matokeo ya hatua zao hizo.

Baada ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina yao na utawala wa Kizayuni unaoikalia Quds kwa mabavu, nchi mbili za Imarati na Bahrain, tarehe 15 Septemba zilijipeleka kwa rais wa Marekani, Donald Trump kwenda kutia saini makubaliano hayo katika ikulu ya White House, sherehe zilizohudhuriwa pia na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, Benjamin Netanyahu.