Zarif: Jamii ya kimataifa lazima iishurutishe Israel iangamize silaha zake za atomiki
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka jamii ya kimataifa iulazimu utawala wa Kizayuni wa Israel usaini mara moja Mkataba wa Kuzuia Usambazwaji Silaha za Nyuklia (NPT) na uangamize maghala yake ya silaha za atomiki.
Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo katika kikao cha Umoja wa Mataifa kilichofanyika kwa njia ya intaneti katika 'Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Kikamilifu Silaha za Nyuklia.' Zarif aliikosoa vikali Marekani na kuitaja kuwa nchi pekee duniani ambayo imewahi kutumia mabomu ya atomiki huku akielezea matumaini kuwa kikao hicho kitaweza kuimarisha mkakati wa kimataifa wa kumuondolea mwanadamu jinamizi la silaha za atomiki.
Zarif ameashiria matakwa ya mara kwa mara ya vikao vya kufanyia marekebisho Mkataba wa Kuzuia Usambazwaji Silaha za Nyuklia na kutokomezwa silaha kama hizo sambamba na ushauri wa Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kuhusu kupigwa marufuku silaha hizo na kusema, madola makubwa yenye silaha za nyuklia yanapaswa kutangaza mpango wenye muda maalumu wa kuangamiza silaha hizo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria hatua ya Marekani ya kuimarisha na kuboresha silaha zake za nyuklia na kusema: "Inasikitisha kuwa, Marekani si tu kuwa inaboresha na kuimarisha silaha zake za nyuklia, bali pia imejipunguzia masharti ya kutumia silaha za nyuklia na inatoa vitisho kwa nchi zingine. Kwa kujitoa katika mapatano ya makombora ya masafa ya kati ya nyuklia na pia mapatano ya nyukli ya JCPOA, Marekani imetoa pigo kubwa kwa mkataba wa NPT."

Zarif pia ameashiria uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao ndio mmiliki pekee wa silaha za atomiki katika eneo la Asia Magharibi na kusema: "Utawala wa Israel ambao ni kawaida yake kuvunja sheria, umetoa vitisho vya kuwaangamiza wengine kupitia silaha za nyuklia lakini wakati huo huo unadai kuwa na wasiwasi kuhusu kuenezwa silaha hizo."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa wito kwa jamii ya kimataifa iulazimu utawala wa Israel, ambao dhati yake ni uvamizi, ujiunge na mkataba wa NPT na ukubali wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki watemblee vituo vyake vya nyuklia.