Rouhani: Uhusiano wa Iran na Kuwait utaendelea kuwa wa kirafiki
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia ujumbe wa pongezi Sheikh Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah, Amiri mpya wa Kuwait.
Katika ujumbe wake huo, Rais wa Iran amelezea matumaini yake kuwa nchi hizi mbili zitaendelea kushuhudia uimarishwaji uhusiano wa kirafiki na kidugu sambamba na ustawi wa uthabiti na usalama katika eneo.
Rais Rouhani amempongeza Sheikh Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah kwa kuchaguliwa kuwa Amir wa Kuwait na amemtakia yeye na watu wa Kuwait mafanikio.
Jana, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifika Kuwaiot na kukutana na kufanya mazungumzo na Amir mpya wa nchi hiyo.
Muhammad Javad Zarif ambaye alifanya safari nchini Kuwait kwa ajili ya kumuwakilisha Rais Hassan Rouhani, aliwasilisha salamu za pole na rambirambi kwa serikali na wananchi wa nchi hiyo kwa mnasaba wa kufariki dunia Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah aliyekuwa amir wa nchi hiyo ambaye aliaga dunia hivi karibuni.
Katika mazungumzo yake na Nawaf Al-Ahmad Al-Jaber Al-Sabah amir mpya wa Kuwait, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kumpa pole kiongozi huyo mpya wa Kuwaita amempongeza pia kwa kuchaguliwa kuwa amir mpya wa nchi hiyo.
Aidha Zarif alimwambia amir mpya wa Kuwait kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo ya Kirabu. Akiwa nchini humo, Dakta Zarif amekutana na kufanya mazungumzo pia na Ahmad Nasser Al-Mohammed Al-Ahmed Al-Jaber Al-Sabah ambaye ni Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Kuwait.
Amir wa Kuwait, Sheikh Sabah al-Ahmad al-Jaber al-Sabah aliaga dunia huko nchini Marekani tarehe 29 ya mwezi uliopita wa Septemba akiwa na umri wa miaka 91 baada ya kuugua.
wakati wa uhai wake Sheikh al-Sabah alifahamika zaidi kama mbunifu wa sera za nje za enzi hizi nchini Kuwait na pia msuluhishi na mpenda amani.