Oct 07, 2020 12:35 UTC
  • Rais Rouhani: Iran haitoruhusu magaidi waweko kwenye mipaka yake

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Tehran kamwe haitoruhusu magaidi waweko kwenye mipaka yake na kuongeza kuwa, jambo hilo halikubaliki kabisa na Tehran imewatangazia waziwazi msimamo wake huo, viongozi wa nchi zote jirani.

Rais Rouhani amesema hayo leo katika kikao cha Baraza lake la Mawaziri na huku akigusia mazungumzo yake na viongozi wa ngazi za juu wa nchi mbili za Armenia na Jamhuri ya Azerbaija amesema, katika mazungumzo hayo kumesisitizwa wajibu wa kulindwa ardhi yote ya Jamhuri ya Azerbaijan lakini Iran inaamini kwamba suala lolote lile haliwezi kutatuliwa kwa njia za vita na mapigano. Vile vile amesisitiza kuwa, kuna wajibu wa kutafutwa njia yingine za utatuzi. Amesema, Tehran iko tayari kufanya juhudi zake zote kutatua kwa njia salama mgogoro wa nchi hizo mbili.

Aidha amesisitiza kuwa, kamwe Iran haitoruhusu magaidi ambao imekuwa ikipambana nao kwa miaka mingi huko Syria, watumie kisingizio chochote kile kuhatarisha usalama wa Jamhuri ya Kiislamu katika mipaka yake.

Mapigano baina ya Armenia na Azerbaijan

 

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha ametahadharisha kuhusu hatari ya kugeuka vita baina ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan na kuwa vita vya eneo hili zima. Amesema, watu ambao wanachochea vita hivyo ili viendelee na vienee katika eneo hili lote wanapaswa kutambua kuwa, jambo hilo si kwa manufaa yao.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa mara nyingine amesisitiza kwa kusema: Lazima juhudi zaidi zifanyike kuhakikisha mgogoro wa Azerbaijan na Armenia unatatuliwa haraka kwa njia za amani.

Tags