Uraibu wa Marekani wa kutoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran
Mapatano ya nyuklia ya Iran na kundi la 5+1 ambayo yalianza kutekelezwa mwezi Januari mwaka huu, yamepelekea kuondolewa kwa vikwazo ambavyo vilikuwa vikitekelezwa dhidi ya nchi hii kwa kisingizio cha mpango wake wa nyuklia.
Licha ya watekelezaji wa siasa za kigeni za Marekani kudai kwamba hakuna kizuizi chochote kinachozuia kuondolewa vikwazo hivyo lakini ushahidi uliopo unaonyesha wazi kwamba mashirika na idara za Marekani zinafanya kila jambo linalowezekana ili kuvuruga uondolewaji wa vikwazo hivyo. Na mfano wa wazi wa suala hilo ni mbinu tofauti zinazotekelezwa hivi sasa na Congress ya Marekani ili kuzuia kuondolewa kwa vikwazo hivyo. Televisheni ya Fox News ya Marekani iliripoti siku ya Jumanne kwamba wanachama watatu wa Congress hiyo waliliandikia barua shirika la utengenezaji ndege la nchi hiyo Boeing wakilionya kwamba aina yoyote ile ya mkataba kati yake na Iran kuhusiana na mauzo ya ndege za shirika hilo itaisaidia Iran katika kile walichokitaja kuwa uungaji mkono wa Iran kwa ugaidi. Vilevile barua hiyo inadai kwamba huenda ndege hizo za abiria zikageuzwa na Iran na kuwa ndege za kivita. Barua hiyo iliyoandikwa kwa Dennis Muilenburg, mkurugenzi mkuu mwandamizi wa Boeing inamtaka azuie maafisa wa shirika hilo kutia saini mkataba wowote wa mauzo ya ndege za shirika hilo kwa Iran. Kwa mujibu wa mapatano ya kuondolewa vikwazo dhidi ya Iran, mashirika ya ndege ya Iran yameondolewa katika orodha ya vikwazo ya Wizara ya Fedha ya Marekani. Kwa mujibu wa mapatano hayo, Iran inaweza kuuziwa ndege za abiria. Ni wazi kuwa shirika la Boeing si shirika pekee la ndege ambalo linafanya juhudi za kunufaika na soko la Iran bali mashirika ya nchi nyingine pia yanafanya juhudi za kunufaika na fursa za kibiashara na Iran. Hata hivyo serikali ya Tehran imetangaza mara nyingi kwamba licha ya kuwa mashirika ya Marekani yana hamu kubwa ya kunufaika kiuchumi na kibiashara na Iran lakini Iran haiipi nchi hiyo kipaumbele kuhusiana na masuala ya kibiashara. Moja ya mambo yanayosisitizwa na Iran kuhusu jambo hilo ni kuzingatiwa miendeno ya kisiasa ya zamani na ya sasa ya nchi tofauti na kiwango cha kuaminika nchi hizo katika jamii ya Iran. Katika mazungumzo yake na Rais wa Korea Kusini hivi karibuni, Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran hata alisisitiza kwamba kutoathirika mapatano na mikataba ya pande mbili na masuala ya nje ni moja ya mambo muhimu yanayozingatiwa katika ushirikiano wa kibiashara wa Iran na nchi za kigeni.
Ni wazi kuwa sababu ya uvurugaji mambo unaofanywa na Marekani dhidi ya Iran sio sheria za ndani ya nchi hiyo wala wasiwasi kuhusiana na masuala ya haki za binadamu na ugaidi bali ni jinsi ya kuipaka matope Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Moja ya madai yanayotolewa na Marekani ni kuwa kwa kuyafanya majaribio makombora yake ya masafa marefu, Iran imekiuka maazimio kadhaa ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Katika hatua nyingine inayokiuka wazi sheria za kimataifa, Mahakama Kuu ya Marekani wiki kadhaa zilizopita ilitoa hukumu ya kunyakuliwa fedha za Iran zinazozuiliwa nchini humo kinyume cha sheria kwa ajili ya kuzilipa fidia familia za askari wa Marekani waliouawa katika mlipuko uliotokea mjini Beirut Lebanon mwaka 1983.
Mfano mwingine wa harakati za kiuadui zinazofanywa na Wamarekani dhidi ya Iran ni ule mswaada uliowasilishwa kwenye bunge la Marekani na James Randy Forbes, mwakilishi wa chama cha Republican katika Congress ya Marekani. Mswada huo unadai kwamba mazoezi ya kijeshi yanayofanywa na Iran katika maji ya Ghauba ya Uajemi yanazidisha mivutano na hivyo kuathiri uthabiti wa eneo na vilevile kuhatarisha usalama wa askari wa Marekani walio katika eneo hilo. Utangulizi wa mswada huo unaitaka serikali ya Marekani kutoa jibu kali kwa kile kimetajwa kuwa ni tabia hatari ya Iran.
Ni wazi kuwa licha ya kwamba tabia ya Marekani katika uwanja huo ni aina fulani ya maradhi, lakini ukweli wa mambo ni kuwa jambo hilo linabainisha wazi utambulisho halisi wa viongozi wa Marekani. Madai yasiyio na msingi ya Marekani dhidi ya Iran kwa hakika yamebadilika na kuwa aina fulani ya uraibu kwa viongozi wa nchi hiyo.