Iran yakanusha madai ya kuingilia uchaguzi wa Marekani, yasema hauna umuhimu kwake
Msemaji wa Ofisi ya Iran katika Umoja wa Mataifa amepuuzilia mbali madai kuwa Jamhuri ya Kiislamu inaingilia uchaguzi wa Marekani.
Alireza Miryousefi amesema hayo katika ujumbe wake wa Twitter usiku wa kuamkia leo na kuongeza kuwa, "kinyume na ilivyo Marekani, Iran haingilii chaguzi za nchi nyinginezo duniani."
Ametaja tuhuma hizo kama senario itakayodhoofisha imani ya wapiga kura katika uchaguzi mkuu wa Marekani unaotazamiwa kufanyika mwezi ujao wa Novemba.
Kauli hiyo ya Miryousefi ni jibu kwa matamshi ya John Ratcliffe, Mkurugenzi wa Idara ya Intelijensia ya Marekani, aliyedai hapo jana kuwa, Iran na Russia zinakula njama ya kuathiri matokeo ya uchaguzi mkuu wa Marekani.
Msemaji wa Ofisi ya Iran katika Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa, dunia imekuwa ikishuhudia namna hata maafisa wa ngazi za juu wa Washington wanavyotilia shaka matokeo ya uchaguzi wao wenyewe.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema taifa hili halijali wala halishughulishwi ni nani ataibuka mshindi katika uchaguzi wa rais wa Marekani.
Mahmoud Vaezi alisema hayo jana pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri hapa Tehran na kuongeza kuwa: Matokeo ya uchaguzi wa rais wa Marekani hayatakuwa na athari yoyote kwa sera zilizo wazi za Jamhuri ya Kiislamu.